Temeke waanza huduma usafishaji damu

DAR ES SALAAM ;Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke(TRRH),  imeanza rasmi kutoa huduma za usafishaji damu (dialysis) leo Juni 14, 2024, ikiwa ni mara ya kwanza kwa hospitali hiyo kutoa huduma hiyo maalumu itakayo hudumia wananchi wenye changamoto ya figo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Joseph Kimaro, amesema ni siku maalum na muhimu kwa hospitali hiyo, kwani huduma hiyo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu.

Amesema wamepata mashine 10 za usafishaji damu zilizonunuliwa kwa kutumia mapato ya ndani na kueleza kuwa huduma hiyo itasaidia wagonjwa wenye matatizo ya figo wanaoishi pia wilaya za  jirani kama vile Kigamboni na Mkuranga ya Mkoani Pwani, ambako huduma hiyo haijafika bado.

Dk Kimaro amesema kuwa utekelezaji wa huduma hiyo sio tu hitaji la Hospitali ya Temeke, bali ni mpango wa serikali unaolenga kufikisha huduma za kibingwa na bingwa bobezi kwa wananchi na kuongeza kuwa huduma hii mpya itapunguza foleni na changamoto za umbali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Ametoa shukrani kwa Mamlaka ya Usimamizi Bandari (TPA) kwa kuwezesha ukarabati wa jengo hilo na kununua televisheni zitakazosaidia wakati wa kutoa huduma.

Amewataka wananchi kuendelea kufanya mazoezi na kufuata ushauri wa madaktari, ili kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kwani dawa zisipotumika kwa usahihi zinaweza kusababisha changamoto za figo.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, Dk Farida Ntonga, ameshukuru uwepo wa mashine hizo na kusema kuwa timu ya madaktari na wauguzi wamepokea mafunzo ya kutosha, hivyo wananchi wawe na imani na wataalamu hao.

Amesema mwaka jana hospitali ilipokea wagonjwa takribani 200, ambao walihitaji rufaa kwenda Muhimbili, lakini sasa kutokana na huduma hiy mpya, rufaa hizo zitapungua na wagonjwa watapata huduma katika hospitali hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button