TFF yapitisha bajeti bil 56/- ya mwaka 2025

MKUTANO Mkuu wa 19 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) umepitisha bajeti ya Sh Bilioni 56.31 kwa mwaka 2025 kutoka katika vyanzo mbalimbali.

Katika bajeti hiyo ya Sh bilioni 56, 306, 464, 295.00 matumizi ni Sh bilioni 56,165,406,168.41 na bakaa ni Sh milioni 141,051,126.59 kiasi ambacho Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia alisema kinaweza kushuka kutokana na mwenendo wa mauzo ya dola ya Marekani sokoni kwa sababu fedha zingine wanalipwa kwa dola.

Kiasi hicho cha bajeti ya 2025 ni tofauti ya Sh bilioni 15.92 na iliyopitishwa mwaka 2024 ambayo yalikuwa Sh bilioni 40.39 lakini shirikisho lilifanikiwa kukusanya Sh bilioni 35.54 ambayo ni sawa na asilimia 88 ya malengo.

Advertisement

Kwa upande wa matimizi shirikisho lilipanga Sh bilioni 40.16 kwa mwaka 2024 lakini hadi Septemba 2024 lilitumia Sh bilioni 35.61 ambayo ni asilimia 87 ya bajeti ya matumizi.

Akifafanua bajeti ya 2025 alisema mapato yatokanayo na viingilio ni Sh milioni 828, kutoka katika klabu Sh bilioni 1.17, mapato ya udhamini sh bilioni 5.03, mapato kutoka haki za matangazo Sh Sh 2.68.

Kadhalika fedha kutoka wafadhali Sh bilioni 9.80, mapato mengine ni Sh milioni 151 na fedha za miradi kutoka Fifa ni Sh bilioni 8.10 kutekeleza Mradi wa kituo cha michezo Mnyanjani Tanga.

Katika kuimarisha kuimarisha ligi TFF inatarajia kupokea Sh bilioni 28.52 kwa upande wa Bodi ya Ligi ambapo kwenye viingilio itapokea Sh milioni 317 ambazo ni kwa ajili ya utawala na upande wa mapato ya udhamini itapokea Sh bilioni 28.02 ambazo zitatumika kulipa usafiri wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu pamoja na waamuzi na mechi zote na mapato mengine itapokea Sh milioni 180.