WAKALA wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) imeweka wazi kuwa imejidhatiti kuimarisha mfumo wa kudhibiti majanga ya moto kwenye maeneo ya hifadhi za misitu kwa kutumia mfumo wa Satelaiti.
Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Rogers Nyinondi amesema hayo mbele ya waandishi wa habari katika shamba la miti Silayo, wilayani Chato wakati wa mafunzo kwa maofisa wa TFS jinsi ya kukabili majanga.
Nyinondi amesema semina na mafunzo hayo yametolewa kwa maofisa 17 wa TFS kanda ya ziwa juu ya matumizi thabiti ya Satelaiti na kuachana ulinzi wa hifadhi za misitu kwa kutumia minara.
Amesema mafunzo yamelenga kuwafanya maofisa wahifadhi wa TFS waweze kuyatambua matukio kwa haraka kwa njia za mtandao, kutambua tukio la moto limetokea sehemu gani na moto unasambaaje.
“Wahifadhi watakuwa na uwezo wa kupokea meseji kwenye simu zao, pale tukio la moto linatokea eneo lao ama jirani na eneo ambalo wanalisimamia, kwani moto unatokea ndani ya hifadhi na nje ya hifadhi.
“Imeonekana matukio mengi ya moto yanaanzia nje ya hifadhi yanaingia ndani ya hifadhi, kwa sababu hifadhi zetu zinapakana na mashamba ya wakulima,” amesema Nyinondi.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Silayo, Juma Msiti amesema pamoja na ujio wa mfumo mpya wa satelaiti lakini wao wameimarisha elimu na ushirikishaji wa jamii inayozunguka shamba la miti Silayo.
“Shamba hili linaendelea vizuri, na mpaka sasa bado lipo vizuri tangu tumeanza hamna tukio lolote la moto limetokea, na hili ni kwa sababu ya mahusiano mazuri na wananchi.
“Wananchi wameelimishwa, wanaelewa kwamba shamba hili ni mali yao, kwani wao asilimia zaidi ya 90 shughuli zote zinafanywa na wananchi wanaozunguka shamba, wanafanya kazi na wanalipwa,” amesema Msiti.
Ofisa Uhifadhi wa TFS Kituo Cha Rubya, Valentine Mosha amekiri kuwa mfumo wa awali wa kutambua matukio ya moto kwa kutumia minara ulikuwa mgumo kwao na sasa satelaiti zitarahisisha zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Lous Bura amewataka wakazi wa Chato wanapoandaa mashamba kuachana na uchomaji holela badala yake wakusanye mabiyu na kuyachoma kwa kuzingatia maelekezo ya TFS.