TFS watakiwa kuimarisha misitu kuvutia watalii

WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) wametakiwa kuimarisha utalii wa misitu Ikolojia kwa kuvilinda na kuviendeleza vivutio hivyo ili kuendelea kuvutia watalii wa ndani na wa kimataifa.

Hatua hiyo ni katika kufikia mpango wa taifa wa kufikisha idadi ya watalii wapatao milioni 5 na mapato ya taifa ya Dola bilioni 6 ifikapo 2025.

Advertisement

Rai hiyo imetolewa na Naibu katibu Mkuu (Utalii),Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkoba Mabula wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wahifadhi wa TFS wanaosimamia utalii katika hifadhi za misitu na vituo vya mali kale kutoka mikoa mbalimbali nchini hii leo.

Amesisitiza mafunzo hayo yalenge kuendeleza mazao ya utalii, ukarimu na masoko,matumizi ya mifumo ya tehama ,usimamizi wa mitandao ya kijamii na uandaaji wa maudhui.

Amesema sekta ya utalii imeendelea kuwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa kwa kutoa fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa sekta zingine kiuchumi.

“Sekta ya utalii imeendelea kuchangia pato la taifa kwa asilimia 17.2 kutokana na fedha za kigeni,huku wageni wakiongezeka kwa mwaka 2023 watalii walifikia zaidi ya milioni 1.8 kutoka watalii milioni 1.5 mwaka 2019 kabla ya janga la Covid 19 sawa na ongezeko la asilimia 18”.