WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS)imeanza kutangaza vivutio vyake vya utalii ndani ya misitu ikiwemo utalii wa Ziwa Duluti ili kuhakikisha wageni kutoka ndani na nje ya nchi wanajionea mandhari nzuri ya utalii wa mazingira asilia ya ziwa hilo.
Hayo yamesemwa wilayani Arumeru na Ofisa Misitu, Anna Lawuo wakati alipozungumzia ujio wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Nchi za Afrika (AAAG) waliotembelea ziwa hilo kujionea vivutio vya utalii vya misitu iliyopandishwa hadhi 23 huku maeneo yanayotekelezwa katika shughuli za utalii yakiwa ni 33 ikiwemo yale yaliyopo ndani ya mashamba ya misitu.
Amesema misitu hiyo imepandishwa hadhi kuwa misitu ya mazingira asilia sababu ni maeneo yenye viumbe adimu visivyopatikana ulimwenguni kote ikiwemo misitu yenye miti adimu yenye wanyama na wadudu wote.
“Tunafanya utalii ulikolojia ikiwemo utafiti na mafunzo na kwa hapa Ziwa Duluti ni sehemu iliyohifadhiwa misitu na ni maarufu kwaajili ya maombi na kufanya utalii wa kutembea msituni, maombi na kutembea ziwani.
Amesema ziwa hilo ni maarufu sana katika kufanya maombi, utalii wa maji , uvuaji samaki na utalii wa maji kwa kutumia makasia ya asilia lakini pia utalii huu hupelekea utulivu wa akili na mwili”
Alisisitiza wageni kutoka ndani na nje wanakaribishwa kutembelea eneo hilo la Duluti na maeneo mengine ya TFS kwa ajili ya kusikia milio ya ndege, utulivu wa akili, kutembea ziwani alitoa rai nyakati hizi za sikukuu kutembelea hifadhi za TFS ili kujione vivutio hivyo.
Naye Mhifadhi Mwandamizi wa Misitu Wilayani Arumeru, kutoka TFS , Peter Myonga amesema katika hifadhi hiyo wanafanya shughuli za uhifadhi mazingira ikiwemo kusimamia shughuli za utalii kwakushirikiana na wananchi.