“This is the New Me!” Zuchu awajibu wakosoaji

DAR-ES-SALAAM : MSANII nyota wa Bongo Fleva, Zuhura Othman Soud maarufu kama Zuchu, ameibua mjadala mkali mitandaoni kufuatia kuachia kwa wimbo wake mpya Amanda, huku akiwajibu vikali mashabiki wanaokosoa mabadiliko ya mwelekeo wake wa kimuziki.
Wimbo huo, uliotayarishwa na S2kizzy, umetolewa katika matoleo mawili clean na explicit na kuwasilisha ladha ya kipekee ambayo imewachanganya baadhi ya mashabiki waliokuwa wakiitegemea sauti ya Bongo Fleva.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zuchu alitoa tamko kali kwa wanaoonesha kutoridhika na kazi yake hiyo mpya, akieleza kuwa yuko huru kubadilika kisanii kadri anavyotaka, bila kulazimika kurudi nyuma ili kumridhisha kila shabiki. “This is the new me. I will be as versatile as I want to be. Na kama unahisi mabadiliko haya hayakufai, nakushauri uniache tu sasa,” aliandika Zuchu kwa msisitizo.
Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya mashabiki kueleza kutopendezwa na mtindo mpya wa wimbo huo, wakidai kuwa umetoka nje ya msingi wa Bongo Fleva waliomzoea.Hata hivyo, Zuchu amesisitiza kuwa huu ni wakati wa wasanii kuvuka mipaka ya kawaida na kuonesha ubunifu zaidi katika muziki. “Nimechoka kuimba vitu vile vile kila siku… Kama unapenda msanii kwa vigezo vya Grammy, feel free kushabikia mwingine,” aliandika.
Zuchu pia hakusahau kuwashukuru mashabiki waliomuunga mkono katika hatua hii mpya, akitoa ujumbe wa matumaini: “I love you. Funga mkanda, maana safari ndo kwanza imeanza.” SOMA: Zuchu ahoji ugawaji tuzo za TMA
Wimbo wa Amanda sasa umeibua mjadala mkubwa: Je, huu ni mwanzo wa hatua ya kimataifa kwa Zuchu, au ni kupotea kwenye misingi ya Bongo Fleva?
jag vill trefa hene