Timu ya Madaktari yatua Manyara kutoa huduma

MANYARA: KUFUATIA mafuriko yaliyotokea katika Mji wa Katesh, Mkoa wa Manyara na Kusababisha vifo vya watu takribani 49 na majeruhi 85 Wizara ya Afya imeratibu upatikanaji wa timu za madaktari kwa ajili ya kuongezea nguvu katika hospitali za Mkoa wa Manyara.
Madaktari hao ambao wametoka katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Singida watatoa huduma bora na haraka zaidi kwa majeruhi.
Mapema leo Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel akiongozana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. John Jingu, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Afya wamewasili katika hospitali ya rufaa ya mkoa huo kuona hali ya utoaji huduma na kutoa pole kwa majeruhi 11 wa maafa ya mafuriko.
Dk. Mollel amesema kuwa Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha wanatoa huduma bora za matibabu ili kuokoa maisha ya watu.
Amesema kuwa hadi sasa hospitali zote ndani ya Mkoa wa Manyara zimepokea na kuhudumia majeruhi 93 na wote wanaendelea vyema na matibabu.
“Huduma zinatolewa vizuri, hakuna kilichokosekana na wagonjwa wanaendela vyema na matibabu, kila kitu kinaenda vizuri kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza jana”. Amesema Dk. Mollel.
Mapema leo asubuhi Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sengida amesema kuwa idadi ya vifo vya watu waliofariki dunia kutokana na mafuriko yaliyotokea imeongezeka kutoka watu 47 hadi kufikia 49 baada ya kupatikana kwa miili mingine miwili.
Hapo baadae Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kufika katika Mkoa wa Manyara kujionea hali ya maafa, kutembelea na kutoa pole kwa majeruhi pamoja na kufanya kikao na watendaji katika kushughulikia maafa ya Katesh.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button