IRINGA: Licha ya mvua kubwa kunyesha, wanachama wa Timu Thamani, jumuiya yenye zaidi ya wanachama 800 ambao ni wasikilizaji wa Redio Ebony FM, walikusanyika kwenye viwanja vya Chuo Kishiriki Mkwawa na kufanya bonanza maalum la michezo lililoonesha mshikamano wao wa kipekee.
Bonanza hilo lililoandaliwa chini ya uongozi wa mtangazaji wa Ebony FM, Eddo Bashir lilikuwa na lengo la kuimarisha uhusiano wa wanachama huku pia likitengeneza fursa ya kuchangisha fedha kwa ajili ya safari yao kuelekea Dar es Salaam.
Wanachama hao wanajipanga kwenda kumfariji mwanachama wa timu thamani hiyo, Mama Zeka, ambaye amepooza kwa zaidi ya miezi tisa sasa.
“Mama Zeka ni sehemu ya jamii yetu. Tumeguswa na hali yake na tumeamua mapema mwezi April tutakwenda Dar es Salaam sio tu kumtembelea, bali pia kumchangia ili kusaidia gharama za matibabu,” alisema Mwenyekiti wa Timu Thamani, Jackson Chengula.
Katika bonanza hilo, kilio kingine kikubwa cha wanachama wa Timu Thamani kilikuwa ni hatua ya Ebony FM kutangaza kwamba hivi karibuni itaondoka hewani, hivyo kutosikika katika mawimbi yao ya kawaida.
Timu thamani ambao ni wadau wa redio hiyo walihoji ni lini redio hiyo itarudi tena hewani na wataweza kuisikiliza tena, wakisema kuwa inawakilisha sauti yao na kuunganisha jamii.
Akijibu maswali hayo, Mkurugenzi wa redio hiyo, Nancy Mfugale, alisema redio hiyo haitapotea moja kwa moja na kwamba mchakato wa kuifanya isikike kivingine unaendelea na utakapokamilika itarudi kwa nguvu zaidi.
“Hata kama redio itazimwa, mipango iko tayari kuleta suluhisho la muda mrefu kupitia Ebony Digital, mfumo wa kisasa wa redio kwa teknolojia ya juu,” alisema Mfugale.
Kwa upande wao, wanachama wa Timu Thamani walieleza dhamira yao ya kuendelea kusaidia jamii na kuhakikisha kuwa sauti yao inasikika.
Mbali na safari ya Dar es Salaam kwa ajili ya Mama Zeka, Katibu wa Timu Thamani, Abubakari Mhema alisema kikundi hicho kimepanga miradi mbalimbali ya kijamii inayolenga kusaidia wenye uhitaji.
“Tunataka si tu kuwa mashabiki wa redio, bali kuwa jamii yenye mshikamano inayosaidiana,” alisema Mhema.