Timu zitumie muda vizuri Ligi Kuu kusimama

LIGI Kuu Tanzania Bara imesimama kwa kipindi cha miezi miwili kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2025 na Michuano ya Mabingwa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) yanayotarajiwa kuanza Februari mosi mpaka 28, mwaka huu.
Hii ni kufuatia taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliyotolewa Desemba 31, mwaka jana kupitia akaunti ya Instagram.
“TPLB inatangaza rasmi kuwa baada ya michezo ya Ligi Kuu ya NBC iliyofanyika Desemba 29, 2024, ligi hiyo itasimama hadi Machi 1, 2025 itakaporejea kwa michezo ya mzunguko wa 17,” ilisema taarifa hiyo.
Sababu ya kusimama kwa Ligi hiyo ni kupisha michuano ya kuwania Kombe la Mapinduzi itakayofanyika kisiwani Pemba na Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), ambazo Tanzania ni moja ya wenyeji wa michuano hiyo.
Jambo ambalo ni sehemu ya mafanikio katika mpira wetu yanayochochewa na ushirikiano mkubwa tunaoupata kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
Licha ya changamoto hiyo ambayo imeikumba ratiba ya Ligi Kuu ya NBC, Bodi imejipanga kuhakikisha msimu wa 2024/2025 unafika tamati kwa wakati kwa mujibu wa kanuni za Ligi, hivyo kutoathiri kipindi cha mapumziko na maandalizi ya msimu wa 2025/2026 kwa klabu zetu.
Aidha, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inaamini klabu zake zitatumia kipindi hiki kufanya marekebisho na maboresho katika vikosi vyake ili kuendana na ushindani mkubwa uliopo kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu.
“Bodi inaitakia kila la kheri timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika michuano tajwa hapo juu huku pia, ikiwatakia kheri ya mwaka mpya 2025 wadau wote wa mpira wa miguu zikiwemo klabu, mashabiki, wadhamini, vyama vya soka vya mikoa, vyama vishiriki na watanzania wote kwa ujumla.”

Ligi kusimama kwa ya miezi miwili ni nafasi nzuri kwa timu kujitathmini, kuimarika na kujiandaa kwa mzunguko wa pili wa ligi. Hasa kwa zile timu ambazo hazipo kwenye nafasi nzuri katika Msimamo wa ligi kuu.
Wakati mashabiki wakisubiri kurejea kwa ligi mwezi Machi, ni muhimu kutambua matokeo chanya yanayoweza kutokana na mapumziko haya na hatua ambazo timu zinapaswa kuchukua ili kuhakikisha zinafanya vizuri mzunguko wa pili.

Kupata nafasi ya kujipanga upya
Likizo inatoa nafasi kwa benchi la ufundi kutathmini mzunguko wa kwanza wa ligi, kubaini mapungufu na kutengeneza mbinu bora za mchezo. Timu zinaweza kutumia muda huu kurekebisha makosa yaliyotokea awali na kuhakikisha wanarudi na nguvu mpya.
Kwa mfano Kengold inashika nafasi ya 16 katika msimamo ikiwa na pointi sita, hivyo inaweza kuitumia nafasi hii kujiimarisha kwa kufanya usajili kabambe.

Kuimarisha viwango vya wachezaji
Wakati wa ligi, muda wa mazoezi makali huwa mdogo kutokana na ratiba ngumu ya mechi. Mapumziko haya yanatoa nafasi kwa wachezaji kufanya mazoezi maalumu ya kuimarisha uwezo binafsi, stamina na mbinu za kiufundi.
Matibabu na kurejea kwa wachezaji waliokuwa majeruhi
Wachezaji wengi huwa wanakumbana na majeraha yanayoweza kuathiri viwango vyao vya uchezaji. Mapunziko marefu ya aina hii yanatoa muda wa kutosha kwa wachezaji hao kupata matibabu na kurejea wakiwa na hali nzuri ya kimwili na kiakili.
Fursa kwa wachezaji wapya kuingia kwenye mfumo
Kwa timu zilizosajili wachezaji wapya katika dirisha dogo la usajili, watatumia muda huu wa kuwaingiza kwenye mfumo wa timu. Hii itasaidia kuboresha mshikamano na maelewano kati ya wachezaji uwanjani.
Baada ya mapumziko, wachezaji na makocha hurudi wakiwa na ari mpya. Hali hii inaweza kuongeza ushindani ndani ya timu, hasa kwa wale wanaopigania namba katika kikosi cha kwanza.
Vilevile hiki ni kipindi muhimu kwa mabenchi ya ufundi kuziandaa timu zao kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu, hivyo wanapaswa kufanya mambo kadhaa ya muhimu kuelekea mzunguko wa pili.

Miongoni mwa mambo hayo ni:
Kuongeza nidhamu na umakini wa wachezaji
Timu zinapaswa kuimarisha nidhamu ya wachezaji ili kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya benchi la ufundi. Nidhamu bora ni msingi wa mafanikio ya muda mrefu.

Kuongeza ushirikiano kati ya makocha na wachezaji
Katika kipindi hiki makocha na wakufunzi watapata muda mwingi wa kukaaa na wachezaji, hivyo inaweza kusaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya makocha na wachezaji huchangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu.
Aidha, mapunziko haya marefu ya Ligi Kuu Tanzania Bara si tu fursa ya mapumziko pekee, bali ni muda wa kuimarisha viwango vya timu na wachezaji. Timu zinazotumia mapumziko haya vyema zina nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi katika mzunguko wa pili.



