TMDA yateketeza tani 3.8 ya dawa zisizo na ubora Geita

OFISI ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Magharibi imeteketeza dawa zenye uzito wa tani 3.8 na thamani ya sh milioni 23.41 zilizokosa ubora mkoani Geita kwa mwaka wa fedha 2024/25.

TMDA Kanda hiyo inayojumuisha Geita, Shinyanga na Kagera imeteketeza vifaa tiba vyenye uzito wa kilo 450 na thamani ya sh milioni 12.8 ndani ya mkoa huo.

Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Magharibi, Dk Edger Mahundi ametoa taarifa hiyo katika ufunguzi wa semina kwa wataalam na watendaji wa afya ndani ya halmashauri zote za mkoa wa Geita.

Dk Mahundi amesema kikao hicho kinalenga kupeana uelewa mbalimbali kuhusu sheria ya dawa na vifaa tiba sura namba 219, ili kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Ameongeza pia miongoni mwa dawa na vifaa tiba zilizokamatwa ni zile ambazo hazijasajiliwa na TMDA, bidhaa duni pamoja na bidhaa za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Katika maduka ya dawa muhimu kumekuwa na ongezeko la dawa za cheti zisizoruhusiwa na kuuzwa katika aina hiyo ya maduka, dawa hizi huondolewa na kugawiwa bure kwenye taasisi zenye uhitaji, ” amesema Dk Mahundi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Lucy Beda amesema suala la usimamizi wa usajili na uuzaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi linapaswa kuwekewa mkazo ili kuokoa maisha ya watu wasio na uelewa.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba.

Kaimu Mkuu wa mkoa wa Geita ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba ameitaka TMDA kusimamia kwa kina malengo ya serikali kuhakikisha ubora wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba unafikiwa kwa kiwango thabiti.

Komba ameagiza hatua ziendelee kuchukuliwa kukomesha uuzaji holela wa dawa na vitendanishi zilizoisha muda wa matumizi na kudhibiti dawa ambazo hazipaswi kuuzwa kwenye maduka ya dawa binafsi.

Aidha ameelekeza TMDA kufuatilia maduka yote yaliyopo kwenye maeneo tofauti iwapo yamepata usajili halali wa TMDA na yanatoa huduma kulingana na sifa na vigezo vilivyotolewa na TMDA.

“Watumishi wa afya ambao mmekasimiwa majukumu na TMDA, nendeni mkawe wazalendo, kwa kuwalinda watanzania, kufanya kaguzi kwa umakini na usahihi.

“Msipotumia wajibu wenu, msipotumia taaluma yenu, msipotumia weledi wenu, mtaliangusha taifa hili na mtawaumiza watu walio wengi”, amesisitiza Komba.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button