Tandahimba wahimizwa matumizi nishati safi ya kupikia

JAMII katika Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara imehimizwa kuendelea kuhamasika juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili iweze kuondokana na nishati zinazoharibu mazingira ikiwemo ukataji miti.
Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Tandahimba Jafari Mwadili ametoa wito huo wakati Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 ulipopitia miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri hiy ukiwemo mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Shule ya Msingi Mji Mpya Maalum.

“Ni vizuri kumuunga mkono Rais wet katika matumizi ya nishati mbadala kwasababu kwa sasa dunia inatutaka twende huko na tuachane na zile nishati zinazoharibu mazingira yetu,” amesema Mwadili.
Amesema viongozi waendelee kuwahimiza wananchi na wadau mbalimbali kuhakikisha nishati hiyo zinaletwa za kutosha na wananchi wanaendelee kuzitumia kwa ajili ya ustawi wa maendeleo na mazingira ya halmashauri kwa ujumla.

Ofisa Tarafa ya Mchichira kwenye halmashauri hiyo, Doto Nyirenda amesema uzinduzi wa nishati hiyo ni faraja kubwa kwake kwasababu ni mkombozi kwa mwanamke na inaokoa muda kutokana akina mama kuwa na majukumu mengi ya kifamilia hivyo itawarahisishia kupika chakula kwa haraka lakini watalinda afya zao.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Isamil Ali Ussi amesema Rais Samia Suluhu Hassan wakati anazindua kampeni hiyo ya utumiaji wa nishati hiyo alielekeza kuwa halmashauri zote, taasisi, wilaya na mikoa zinazowahudumia wananchi zaidi ya 100 lazima zitumie miundombinu hiyo ambapo sasa wamekuja kujionea kwa macho yao ndani ya shule hiyo.

“’Dk Samia Suluhu Hassan leo hii amekuwa kinara ndani ya Afrika na dunia juu ya uhamasishaji wa matumizi wa nishati safi na salama na leo hii mikutano mikubwa ya dunia inafanyika nchini kwetu na yeye ameibeba sera hii na kampeni ya utumiaji wa nishati safi ndani ya taifa letu,”’amesema Ussi.
Amesema anaamini kampeni hiyo inaendelea kufanikiwa kwa asilimia 100 na malengo aliyojipangia Rais Samia ni kwamba ifikapo mwaka 2030 zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wawe tayari wanatumia nishati hiyo.



