TPA: Uwekezaji bandarini umejikita kiteknolojia

GEITA; MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imebainisha kwamba uwekezaji unaoenda kufanyaika kwenye bandari unalenga kuboresha teknolojia na ufanisi wa upakuaji na upakiaji wa mizigo.

Ofisa Utekelezaji wa TPA, Denis Mapunda amebainisha hayo kwa waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho ya sita ya kimataifa ya teknolojia ya madini katika viwanja vya Bombambili mjini Geita.

Mapunda amesema watu wanapaswa kuelewa mbali na mkataba wa uwekezaji bandarini, eneo la gati ya bandari litabakia kumilikiwa na serikali lakini mwekezaji atakuja kuweka mitambo kwa ajili ya kuboresha huduma.

“Kwa hiyo tunatarajia kwamba mwekezaji atakuja na mitambo mingi zaidi kwa sababu meli moja inahitaji mitambo mitatu mpaka minne kupakua mzigo, inategemea ukubwa wa meli.

“Tayari tumeshaongeza kina cha bandari na tumeshafungua mlango kwa mita 60 kwenda chini kwa hiyo tunapokea meli zenye uwezo wa kubeba kontena nyingi zaidi, ambao ni mzigo wa meli zile za tani 60,000.

“Mara ya mwisho tulikuwa na tani 40,000 leo tumeongeza kina sasa tutaweza kupokea meli za tani 60,000 katika bandari zetu

“Kwa hiyo mzigo ni mkubwa na tunahitaji uwekezaji mkubwa, ambapo mtambo mmoja ni Shilingi bilioni 51, ambapo tunahitaji mitambo mingi kuanzia gati namba saba mpaka gati namba 12,” amesema.

Amesema maboresho hayo yanatarajiwa kufanyika kwenye Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mtwara pamoja na bandari ya Tanga, ili kuongeza ufanisi wa kutoa huduma kwa meli nyingi zaidi ndani ya muda mfupi.

Habari Zifananazo

Back to top button