TPA yaagizwa usimamizi ujenzi matangi ya mafuta

SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imsimamie mkandarasi anayejenga matangi 15 ya kuhifadhia mafuta ili mradi huo utekelezwe kwa viwango na ukamilike kwa wakati.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alitoa agizo hilo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.

default

Profesa Mbarawa alisema ujenzi wa mradi huo umefika asilimia 14.7 kutoka asilimia tano Septemba mwaka jana.

Advertisement

Mradi huo una thamani ya Sh bilioni 678.6 na unatekelezwa kwa miaka miwili na ujenzi wake ulianza Agosti 2024 na utakamilika Agosti 2026.

Profesa Mbarawa alisema yanajengwa matangi yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta mita za ujazo 378,000.

Matangi hayo yatahifadhi petroli, dizeli, mafuta ya ndege na moja litakuwa la ziada kwa ajili ya mahitaji ya aina ya matufa yatakayohitajika.

“Mradi huu umefikia asilimia 14.77, wengi watajiuliza asilimia 14.77 ziko wapi, kazi kubwa ya ujenzi wa mradi huu
unaanza kwa kazi ya msingi, hapa tuliposimama ndipo tunakuja kujenga matenki yetu sasa kabla ya kuyajenga ni lazima uhakikishe udongo uko vizuri,” alisema Profesa Mbarawa.

Aliongeza, “ardhi hii iko sawa sawa kwa ajili ya ujenzi , kwa sababu yamechimbwa mashimo manne yameenda chini meta 28 kuhakikisha zile layers (tabaka) za ardhi ziko stable (imara) na wameona ardhi sasa iko sawa sawa kwa ajili ya ujenzi wa matenki”.

Profesa Mbarawa alisema matangi hayo yataiwezesha nchi kuwa na uwezo wa kuhifadhi mafuta ya kutosha na yatawezesha kupunguza bei za mafuta kwa kuwa tozo zinazotozwa kwa sasa kwenye meli zinazosubiri kupakua mafuta zinaingizwa pia kwenye gharama za mafuta kwa mlaji.

Alisema mradi huo utaongeza ufanisi wa bandari na kupunguza foleni ya meli za kupakua mafuta. Alisema meli
hutozwa fedha nyingi kwa siku ikiwa kwenye foleni ya kusubiri kushusha mafuta bandarini.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *