TPL wamuomba Rais Samia kuingilia mgogoro wa uongozi

MGOGORO wa kiuongozi ndani ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) umechukua sura mpya baada ya kundi la viongozi wa chama hicho jana kutoka mikoa mbalimbali nchini kufika katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakiwa na mabango, wakimlilia Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati kutatua mvutano huo uliodumu kwa muda mrefu.

Viongozi hao wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Dominata Rwechungura, walieleza kuwa wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kushindwa kupata majibu ya hoja zao kutoka kwa Msajili licha ya ahadi za mara kwa mara.

Mgogoro huo unadaiwa kuanza kufuatia mkutano mkuu wa chama uliofanyika Februari 2,2025 ambapo wajumbe kutoka zaidi ya mikoa 20 walidai kutoshirikishwa na kutopata taarifa za mkutano huo.

Katika mkutano huo, Richard Lyimo alijipitisha kuwa mgombea pekee wa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa, kinyume na hali ya awali ambapo wagombea walikuwa watano.

Viongozi hao wamesema kuwa wamejaribu kutafuta suluhu kupitia taasisi mbalimbali zikiwemo TLS (Chama cha Wanasheria Tanganyika) na Tume ya Haki za Binadamu, lakini bado hawajapata mwafaka wowote. Wamesisitiza kuwa msimamo wao si dhidi ya mtu binafsi, bali ni kutafuta haki na kuhakikisha chama kinazingatia misingi ya demokrasia.

“Tumechoka kusubiri majibu ya maneno matupu kutoka kwa Msajili. Tunamuomba kwa dhati Mheshimiwa Rais Samia aingilie kati atusaidie kumaliza mgogoro huu ili chama kiweze kufanya kazi zake kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi,” alisema mmoja wa viongozi hao.

Tangu kufariki kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa TLP, Hayati Augustine Mrema, chama hicho kimekumbwa na mivutano ya kiuongozi.

Hali hiyo imezua mkanganyiko wa mara kwa mara kuhusu uhalali wa viongozi wanaoendelea kushikilia nafasi za juu ndani ya chama.

Kwa sasa, viongozi hao wanaamini kuwa suluhu ya mwisho ipo mikononi mwa mamlaka ya juu ya nchi, wakimtazama Rais Samia kama kimbilio la mwisho katika kutafuta haki yao ndani ya TLP.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button