TPLB na ramani ya Ligi Kuu msimu ujao 2025/2026

UWEZO wa kupanga mikakati na kuitekeleza una faida nyingi ambazo zinasaidia katika kufikia malengo na kuhakikisha mafanikio lukuki.

Kama vile kutoa maelekezo ya wazi kuhusu ni hatua gani zitachukuliwa malengo fulani yasipofikiwa, hii inasaidia timu kuelewa nini cha kufanya na lini, na hivyo kuepuka mkanganyiko.

Katika nadharia hiyo ya kupanga mikakati na kuitekeleza hivi karibuni, Desemba 7, mwaka huu Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilifanya mkutano wake mkuu wa 11, mkoani Kigoma.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuweka mikakati ya namna Ligi Kuu Tanzania Bara inavyopaswa kuwa msimu wa 2025/ 2026.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo alisema moja ya nguzo muhimu ya bodi hiyo ni Mkutano kama huo unaofanyika mara moja kwa mwaka, kwani ndio wenye maamuzi ya mwisho kwenye usimamizi
na uendeshaji wa ligi zote tatu; Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Ligi ya Championship na First Division League.

Huku uwakilishi wake ukitekelezwa kupitia wenyeviti wa vilabu vyote 16 vya Ligi Kuu, vilabu 16 vya Ligi ya Championship pamoja na uwakilishi wa vilabu vinne vya First League. Mgeni rasmi katika mkutano huo, Wallace Karia ambae pia ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) alisema shauku kubwa ni kuona ligi inakuwa bora zaidi.

Alitaja maeneo ambayo watayazingatia bila kupepesa macho kuwa ni suala zima la udhamini, viwanja vya mazoezi, makocha wageni pamoja na utawala bora. Pia, aligusia nafasi ya waamuzi, video za usaidizi kwa waamuzi (VAR) pamoja na ufanisi wa tiba kwa wachezaji.

Alisema mpira wa Tanzania utakua kwa kusimamia mambo ya muhimu ambayo anaamini yanatekelezeka. Alisema msimu ujao lazima kila timu ihakikishe inamiliki uwanja wa mazoezi kwani hiyo ni moja ya sharti kuu la Leseni ya Vilabu, na kudai kuwa klabu ambayo haitatekeleza ni wazi imedhamiria kujitoa kwenye ligi bila kujali ubora wa matokeo yake.

“Kumiliki kiwanja cha mazoezi sidhani kama ni jambo linalochukua miezi sita, ni lazima litekelezwe na ninyi wenyewe pia ‘waandishi wa habari’ muwe wakweli muwaambie, muwaseme, msichukue tu mambo yanayoleta taharuki, ni vizuri muwaambie mambo ya msingi haya,” alisema Karia.

Alifafanua kuwa viwanja vya kuchezea kanuni zipo wazi kuwa si kigezo cha lazima ili kutimiza matakwa ya leseni hiyo. Huku TFF ikiweka mkakati kwa kushirikisha wadau wa soka kuhakikisha ubora wa viwanja ili kutokomeza
kasumba ya kufungia viwanja kutokana na ubora duni.

Pia, kutimiza dhana ya timu za mikoani kutohama kwenda mkoa mwingine kufuata uwanja wa kuchezea. Jambo lingine linalopigiwa chapuo kwenye ligi msimu ujao ni kuwavutia wadhamini wa kutosha.

Karia alisema wanahitajika wadhamini wengi ili ligi izidi kuwa bora, kwani mafanikio yaliyopatikana yamechangiwa na uwepo wao, hivyo angependa kuona idadi inaongezeka zaidi hasa kwenye ngazi ya vilabu. “Kwenye ligi yetu bado
tunahitaji wadhamini zaidi, kwani ligi bila udhamini haifiki popote hivyo kama kuna dosari na mnaiona basi mwenye ushahidi awasilishe,” alisema Karia.

TFF pia imeazimia kuanzisha utaratibu wa kutoza ada kwa makocha wageni pamoja na wasaidizi wao kama ilivyo sasa kwa wachezaji wageni. Sababu ya kufanya hivyo ni kudhibiti ubora wa makocha wa kigeni na wasaidizi wao kwani wamebaini baadhi yao hawana sifa hizo kuliko wazawa.

Pia, alieleza itakuwa chanzo cha mapato akilinganisha na jinsi ada za wachezaji wageni zinavyoongeza mapato
katika shirikisho hilo na kwamba kiasi cha ada hiyo kitawekwa wazi siku zijazo. Kwa upande mwingine mfumo wa matumizi ya teknolojia ya usaidizi wa uamuzi kwa njia ya video (VAR) hautaanza karibuni licha ya mafunzo yanayoendelea kutolewa kwa baadhi ya waamuzi.

Karia alidai kukosekana kwa miundo mbinu bora ya viwanja, uchache wa mitambo hiyo pamoja na kutomudu kuinunua kwa wakati ni sababu zinazochelewesha kuzitumia. Huku kukiwa na uwezekano wa kuchukua muda
hadi wa misimu miwili ya ligi hiyo kabla ya kuanza matumizi yake.

“Hatuna miundombinu bora ya viwanja ambayo inaweza kuruhusu kutumia VAR katika kila mechi za Ligi Kuu Tanzania zitakazochezwa, ingawa tukifanikiwa kuweka sawa basi tutaanza kutumi,” alisema Karia.

Aliongeza: “tunaongea na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuangalia namna ya kupata VAR za bei nafuu ambazo zinalingana na miundo mbinu yetu, hatusemi ni lini tutapata na kuanza kutumia lakini ndani ya miaka miwili hivi tuna imani itakuwa vizuri.”

Naye Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto alisisitiza kuwa kipaumbele ni ligi bora. “Tunachofanya sasa ni kuangalia ligi yetu tutaiboreshaje msimu ujao, na tutakachofanya ni kuhakikisha maazimio yote tunayafuatilia kwa utekelezaji, nia ni kukidhi matakwa ya Leseni za Vilabu kwa asilimia 100,” alisema Mnguto.

Huku akisisitiza kila klabu lazima kiwe na uwanja wa mazoezi, na kwamba uwanja wa mazoezi ni tofauti na uwanja wa kuchezea mechi.

Habari Zifananazo

Back to top button