MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA) ofisi za Geita imeendesha semina kwa wafanyabiashara wa Busolwa wilayani Nyang’hwale iliyolenga kuondoa dhana potofu na utata juu ya masuala mbalimbali ya kodi.
Akizungumuzia semina hiyo, Ofisa Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA Mkoa wa Geita, Justine Katiti amesema semina hiyo ni mwendelezo wa mpango wa TRA kuwafikia wafanyabiashara wa maeneo yote.
Katiti ametaja miongoni mwa maeneo makubwa yanayozingatiwa ni kukutana na wafanyabiashara kusikiliza kero za kikodi na kuwafahamisha wafanyabishara kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi.
Amesema ili wafanyabiashara watambulike na waendelee kufanya biashara kwa uhalali ni lazima warasimishe biashara zao kwa kupata Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) na kuanza kulipa kodi.
Katiti amewaomba wafanyabiashara ili kuepuka malalamiko kwenye makadirio ya kodi zao ni vyema wajidhatiti katika utunzaji wa kumbukumbu za biashara na kutoa risiti za Mashine za Kielektroni (EFD).
Ofisi za TRA zipo wazi na tupo tayari kusikiliza kero za kikodi na kuzitatua kwa haraka ili kujenga mazingira bora ya kufanya biashara”, amesema na kuongeza;
“Ili kufanikisha hili tumetenga siku ya Alhamisi kila wiki kuwa ni siku maalum ya kupokea maoni na kero za kodi kutoka kwa wafanyabiashara hivo wafanyabiashara watumie fursa hii”, amesema Katiti.
Katiti amewataka wafanyabiashara kuondoa dhana potofu juu ya kodi badala yake waichukulie kama sehemu ya kusaidia maboresho ya huduma za kijamii ikiwemo elimu, maji, umeme na barabara.
Baadhi ya wafanyabiashara wa Busolwa wilayani Nyanghwale wamekiri kuguswa na elimu ya TRA kwani kwa muda mrefu wamekosa ulelewa sahihi wa kikodi kutokana na eneo la kuwa nje ya mji.