MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA, Mkoa wa Kikodi wa Kariakoo imezindua kampeni maalum kwaajili ya kuhamasisha matumizi mazuri ya mashine za kieletroniki (EFD) kwa wafanyabiashara nchini.
Kampeni hiyo imeambatana na ubandikaji wa stika maalum za kuhamasisha wafanyabiashara kutoa risiti pale wanapouza bidhaa zao na wananchi kudai risiti ambayo itakuwa thamani sawa na bidhaa waliyonunua kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Meneja Msaidizi wa ukaguzi TRA Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Thoddy Beyanga amesema kuwa wamebaini kuporomoka kwa utoaji wa risiti kwa sababu zinazotolewa zimekuwa tofauti na matarajio na kusababisha kushuka kwa makusanyo kushuka.
Beyanga amefafanua kuwa faida za kutoa na kudai risiti pale biashara inapofanyika husaidia kutunza kumbukumbu na katika ukadiliaji wa mapato yanayoendana na uhalisia wa biashara pamoja na kuchangia pato la taifa.
Amesema kampeni ya uhamasishaji wa wafanyabiashara kutoa risiti na wananchi kudai risiti ni endelevu hivyo jamii inatakiwa kutekeleza bila shuruti.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Boss Shopping Centre, Hanif Janmohamed amesema TRA inapaswa kuendelea kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa kutoa risiti halali kulingana na bidhaa iliyonunua.
“TRA sasa hivi wanafanya vizuri, hakuna ‘Harassment’ kama ilivyokuwa zamani, sasa hivi maisha yanakwenda vizuri, pia tunaelimishana kwenye sehemu ambazo zinachangamoto.” amesema Janmohamed.
Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi na kuelezea kuwa kutoa na kudai risiti ni wajibu wa kila mmoja.
Comments are closed.