TRA yaja na Shahada ya Uzamili ya Kodi kuongeza wataalamu

DAR ES SALAAM: CHUO cha Kodi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA-ITA), kimeanza mchakato wa kuanzisha Shahada ya Uzamili ya Kodi (Masters Degree in Taxation), itakayolenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa vitendo unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari nchini.
Akizungumza katika kikao cha ushirikishwaji wa wadau mbalimbali kilichofanyika chuoni hapo leo Mei 19, 2026 , Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi wa TRA-ITA, Dk Lewis Ishemoi amesema lengo la mkutano huo ni kukusanya maoni kutoka kwa wadau wa ndani na nje ya TRA ili kusaidia kuandaa mtaala unaoendana na mazingira halisi ya soko.
Amesema wadau walioshirikishwa wanatoka katika sekta mbalimbali zikiwemo taasisi za kodi, kampuni binafsi, wataalamu wa sera pamoja na waajiri ili kuhakikisha programu hiyo inazalisha wahitimu wenye uwezo wa kuingia moja kwa moja katika soko la ajira.
“Tunataka kutengeneza mtaala ambao utajibu matakwa ya soko. Ndiyo maana tumewaalika wadau mbalimbali wenye uzoefu kwenye masuala ya kodi, sera na sekta binafsi ili kutoa mawazo yao,” amesema.
Dk Ishemoi amesema tofauti kubwa ya programu hiyo na nyingine zilizopo ni kuwa itakuwa na mwelekeo wa vitendo zaidi, kwa lengo la kumwezesha mhitimu kufanya kazi kwa ufanisi mara tu baada ya kuhitimu.
Amesema hatua ya sasa ni ya kwanza katika mchakato wa kuanzisha programu hiyo, ambapo chuo kinaendelea kushirikisha wadau kabla ya kuingia katika hatua nyingine za maandalizi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Uzamili TRA-ITA, Praygod Chao amesema uamuzi wa kuanzisha shahada hiyo umetokana na uhitaji mkubwa wa wataalamu wenye utaalamu maalumu katika masuala ya kodi.
Amesema kabla ya kuanza maandalizi ya programu hiyo, chuo kilifanya tathmini ya mahitaji ya soko la ajira (Training Neds Assessment) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Ameongeza kuwa programu hiyo itanufaisha watumishi wa TRA, kampuni za ukaguzi wa hesabu, kampuni za kodi pamoja na mashirika mbalimbali yanayohitaji wataalamu wa kodi wenye ujuzi wa juu.
Naye mdau wa Kodi (tax partner) kutoka Kampuni ya Ernst & Young, Donald Nsanyiwa, amesema ushirikishwaji wa sekta binafsi katika maandalizi ya programu hiyo ni hatua muhimu itakayosaidia kuhakikisha mtaala unaandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya waajiri.
Amesema wadau kutoka sekta binafsi wanatarajia kuona programu hiyo ikitoa wahitimu wenye uwezo wa kukidhi changamoto za kisasa katika masuala ya kodi.
“Tunapongeza kuona wameamua kutushirikisha sisi wadau wa nje ili kutoa mawazo yetu. Hii itasaidia kuhakikisha programu itakayokamilika inakidhi mahitaji ya sekta binafsi” amesema.



