MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Geita imewahimiza wafanyabiashara kutumia kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka 2025 kufika Ofisi za TRA ili kufanyiwa na kukamilisha makadirio ya kodi kwa wakati.
Ofisa Mkuu wa Kodi-Idara ya Elimu na Mawasiliano, Justine Katiti amesema hayo wakati akitoa semina na elimu ya mlipa kodi kwa wafanyabiashara wa eneo la Nkome, Wilaya ya Geita mkoani hapa.
Katiti amesema hatua ya kufika mapema kwenye kwa ajili ya makadirio ya kodi kutaondoa msongamano na kuongeza ufanisi wa makadirio ya kodi kwa kila mfanyabiashara ili kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima.
Amewakumbusha wafanyabiashara kutambua kuwa kodi ya mapato inalipwa kila mwaka kwa kufuata mwaka wa kalenda ambapo makadirio hufanyika kuanzia mwezi Januari hadi Machi kwa kila mwaka.
“Changamoto ni kwamba wafanyabiashara wengi wanakuja kufanya makadirio kwenye tarehe za mwisho wa mwezi Machi, na hivo kuweka msongamano mkubwa na matokeo yake kuchelewa kupata huduma kwa wakati,” amesema Katiti.
Aidha amewatoa hofu wafanyabiashara na kuwahakikishia kuwa makadirio yanayofanyika yatazingatia kanuni, taratibu na sheria zinazosimamiwa na TRA na siyo kwa matakwa ya mtu binafsi hivo wasisite kufika ofisi za TRA.
Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la Nkome walioshiriki semina hiyo wameipongeza TRA kwa elimu inayotoa kwani inawakumbusha wajibu wa mlipa kodi na kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza kwa kutotekeleza sheria.