KAGERA:MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kagera imekusanya Sh bilioni 92.3 kwa kipindi cha Julai – Desemba sawa na asilimia 114 ukilinganisha Sh bilioni 80.9 zilizopangwa kukusanywa.
Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Castro John ametoa taarifa hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa kwenye Maadhimisho ya 14 ya Siku ya Shukrani kwa Mlipakodi ambapo amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 TRA kupitia kwa wafanyabiashara, wawekezaji na vituo vya forodha wanapaswa kukusanya Sh bilioni 164.
Akitoa taarifa ya makusanyo kwa kipindi cha miaka mitano amesema kuwa kwa sasa kuna uelewa mkubwa katika maswala ya ukusaji wa kodi na wafanyabiashara wengi wanajua muda wao na kulipa kwa hiari kodi zao ambapo mwaka 2020/2021 mkoa ulipanga kukusanya Sh bilioni 71.05 na walikusanya Sh bilioni 73.3 sawa na asilimia 103.
Amesema mwaka 2021/2022 malengo ilikuwa ni kukusanya Sh bilioni 81.9 zikakusanywa Sh bilioni 94.8 sawa na asilimia 115,mwaka 2022/2023 malengo ilikuwa ni kukusanya Sh bilioni 125.3 zilikunywa Sh bilioni 113 sawa na asilimia 90.2, mwaka 2023/2024 zilipangwa kukusanywa Sh bilioni 118.1 zilikusanywa Sh bilioni 119 sawa na asilimia 101.
“Ukiangalia malengo ya mkoa huu yanaongezeka na jukumu la kukusanya mapato ni la kwetu sote hasa ushirikiano mkubwa, uzalendo, uwajibikaji ili kuendelea kujenga misingi mizuri ya nchi yetu kujitegemea kupitia kodi zetu,tunahitaji ushirikiano wa wadau wetu ili kukamilisha lengo letu la ukusanyaji wa Bilioni 164 kwa mwaka huuu wa fedha 2024/205,”amesema John.
Alitaja baadhi ya mikakati iliyofanya malengo ya kodi kukamilikuwa kuwa ni utoaji wa risiti za kielektroniki, utoaji wa elimu ya ulipaji kodi, ukaguzi wa ritani za kodi, usimamizi wa maadili ya watumishi, kusimamia matumizi ya mifumo ya kodi, kuongeza wigo wa usajili wa wafanyabiashara .
Alitaja changamoto ambazo zinaweza kukwamisha na kupoteza kodi mkoani Kagera kuwa ni kujificha katika mwavuli wa umachinga,ufunguaji holela wa biashara pamoja na wafanyabiashara kutoa listi za kielekroniki zisizo halali.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa pamoja na pongezi nyingi kwa TRA na wadau katika ukusanyaji wa mapato na mabadiliko makubwa ya kodi alisema kuwa watu wanaokwepa kodi wanapaswa kupigwa vita na kuchukuliwa hatua za kisheria haraka.
Hata hivyo aliwataka TRA kuimarisha Doria mipakani,kusimamia maadili ya wafanyakazi,kushughulikia malalamiko haraka ,kuimarisha kumbukumbu za walipa kodi,uwekaji wa mifumo vizuri juu ya ulipaji kodi ili wafanyabiashara wasisumbuke na kuendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi katika maeneo yote.
Sherehe za shukrani kwa mlipa kodi ziliambatana na utoaji wa vyeti wa wafanyabishara waliolipa kodi zao vizuri pamoja na utoaji wa mahitaji maalumu yenye thamani ya shilingi milioni 5 katika kituo cha watoto Yatima UYACHO kilichopo manispaa ya Bukoba.