TRA yataja sababu 8 kuvunja rekodi makusanyo 2024

DAR ES SALAAM; MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetaja sababu nane za ufanisi wa makusanyo ya mapato ya Sh trilioni 16.528 yaliyokusanywa kuanzia Julai hadi Desemba kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Aidha, kwa Desemba 2024 pekee mamlaka hiyo imevunja rekodi ya kukusanya mapato ya Sh trilioni 3.587 kiwango cha juu kabisa kukusanywa kwa mwezi mmoja tangu kuanzishwa kwa TRA.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alitaja sababu hizo nane kuwa ni pamoja na kusimamia ulipaji kodi wa hiari kwa walipakodi nchini pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zao.

Advertisement

Pili, kusimamia ushirikiano baina ya TRA, wizara, taasisi na ofisi nyingine za serikali kusimamia sera za kodi na ufanyaji wa biashara nchini, kuongezeka kwa utendaji kazi mzuri, nidhamu na ubunifu kwa watumishi wa mamlaka hiyo.

Tatu, kuhakiki taarifa za walipakodi kwenye mifumo kabla ya mlipakodi kuwasilisha ritani yake ya kodi, kupitia na kuhakiki akaunti zote za walipakodi wenye marejesho ya malipo ya kodi ya ongezeko la thamani.

Nne, kufuatilia kwa ukaribu hali ya ufanyaji biashara nchini kwa kusimamia kikamilifu uzalishaji wa viwandani na kuendelea kuhimiza matumizi ya mashine za kieletroniki (EFD), matumizi ya mifumo ya ndani ya Tehama na uanzishwaji wa ofisi ya walipakodi binafsi wenye hadhi ya juu.

Sababu ya tano ni uboreshwaji wa mifumo ya Tehama inayosimamia shughuli za forodha kama vile Mfumo wa Usimamizi wa Forodha (TANCIS) na Mfumo wa Dirisha Moja la Pamoja (TeSW) na kuhakikisha inasomana na mifumo ya bandari.

Sita, kuendelea kuboresha mahusiano na wafanyabiashara kwa kutenga siku ya Alhamisi ya kila wiki kuwa ni siku maalumu ya kusikiliza  walipakodi kupitia ofisi zote za TRA nchini na Desemba  ni mwezi wa kutoa shukrani kwa walipakodi wote nchini.

Aidha, sababu ya saba ni kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini uliosababisha kuongezeka kwa shehena ya mizigo inayoingizwa au kuondoshwa nchini katika vituo vya forodha na huduma zitolewazo bandarini.

Akifafanua makusanyo ya kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, kuanzia Oktoba hadi Desemba 2024, Mwenda alisema wamekusanya Sh trilioni 8.741 sawa na ufanisi wa asilimia 104.63 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 8.354.

Mwenda alisema makusanyo hayo ni ukuaji wa asilimia 19.05 ukilinganisha na Sh trilioni 7.342 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2023/2024.

Kuhusu makusanyo ya Desemba 2024, Mwenda alisema TRA imevunja rekodi tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo kwa kukusanya Sh trilioni 3.587 sawa na ufanisi wa asilimia 103.52 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 3.465.

Alisema makusanyo yaliyokusanywa katika robo ya pili ya mwaka 2024/2025 yameifanya TRA kuwa imekusanya Sh trilioni 16.528 katika nusu ya kwanza (Julai – Desemba 2024) sawa na ufanisi wa asilimia 104.76 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 15.778.

“Makusanyo haya ni ukuaji wa asilimia 18.77 ukilinganisha na Sh trilioni 13.917 zilizokusanywa mwaka wa fedha 2023/2024 na TRA imeandika rekodi mpya ya kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi sita mfululizo katika nusu ya kwanza (Julai – Desema 2024/2025),” alisema Mwenda.

Akifafanua hilo, alisema makusanyo yaliyokusanywa Julai hadi Desemba 2024/2025 ya Sh trilioni 16.528 ni kiwango cha juu kabisa kufikiwa na makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 78.78 kutoka Sh trilioni 9.242 zilizokusanywa mwaka 2020/2021 kabla ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema kwa makusanyo hayo ni kiashiria chanya cha kufikia lengo la makusanyo kwa mwaka 2024/2025 ambayo TRA imelenga kukusanya Sh trilioni 30.04.

Ili kufikia lengo hilo, Mwenda alisema TRA imejipanga kutekeleza maagizo manane mengine ambayo ni kutekeleza maagizo yote ya Rais Samia kuhusu usimamizi wa kodi nchini na ulipaji wa hiari.

Kuanza matumizi ya Mfumo wa TANCIS ulioboreshwa na Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) kuanzia Januari mwaka huu, kuendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano wa walipakodi na utoaji huduma bora, kuimarisha usimamizi wa utoaji risiti za EFD na kufanya kampeni mbalimbali.