TRA yataka wafanyabiashara wasiogope kodi
GEITA; MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Geita, imewataka wafanyabishara kufanya biashara zao bila woga wa sheria ya kodi, badala yake wazingatie sheria kwa kulipa kodi kuchangia mapato serikalini.
Ofisa Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano TRA Mkoa wa Geita, Justine Katiti amebainisha hayo alipokutana na wafanyabiashara Kata ya Muganza wilayani Chato kuhamasiha kampeni ya Tuwajibike.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dk Samia Suluhu Hassan inatamani kuona kila sekta ikiwemo sekta ya biashara inakua na hivo wafanyabiashara wawe huru na wazingatie sheria za nchi.
Katiti amesisitiza wafanyabiashara hao kuliwekea mkazo suala la kutunza kumbukumbu za biashara zao na kudai risiti za manunuzi, kutoa risiti za Mashine za Kielektorniki (EFD) kwa kila mauzo.
Amesema utunzaji wa gharama wanazotumia kwenye biashara zao inaweka msingi bora wakati wa kufanyiwa makadirio ya kodi, kulipa kodi stahiki na kupunguza migogoro ya kodi na kukuza biashara zao.
Amewakumbusha kuwa madhara ya kutotoa au kudai risiti yanasababisha serikali kupoteza mapato yake na hivyo kurudisha nyuma mipango ya serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Katiti amewashauri pia wafanyabiashara kurasimisha biashara zao kwa kufika TRA na kujisajili kwa kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), ikiwa ni utambulisho wa biashara zao kisheria.
Mwenyekiti wa Kata ya Muganza wilayani Chato, James Mpanduji alikiri kampeni ya Tuwajibike inayoratibiwa na TRA imewaleta pamoja wafanyabisahara, wananchi na serikali kwa ujumla.
Amesema kupitia kampeni hiyo wamekumbushwa wajibu wao kama walipakodi na madhara ya kutofuata sheria za kodi ikiwemo kutotoa risiti za EFD na kuahidi kuendelea kuiunga mkono TRA.