TRC yachomoza kongamano la reli Afrika Kusini

Shirika la Reli nchini (TRC),  limeshiriki kongamano na maonesho ya 11 ya Mashirika ya Reli katika Ukanda wa SADC, yanayoendelea jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Kongamano na maonesho ya mwaka huu yamebeba ujumbe unaolenga ubunifu katika mabadiliko ya teknolojia za uendeshaji wa reli, ambapo pamoja na Tanzania inayowakilishwa na TRC, mataifa mengine ni wenyeji Afrika Kusini, Botswana, Eswatini, Msumbiji, Angola, DRC, Malawi na Zambia.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa kongamano hilo, mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa TRC, Amina Lumuli, ameeleza kuwa Tanzania imethibitisha kuwa mbele katika mipango ya mageuzi ya usafirishaji kwa njia ya reli kusini mwa Afrika kama ujumbe wa kongamano la mwaka huu unavyosisitiza.

“Kupitia SGR ukilinganisha na mataifa mengine ya ukanda huu, tunaonekana tuko mbele zaidi kwa ujenzi wa miundombinu hii ya kisasa, ambayo itasaidia sana katika kupunguza muda wa safari na ufanisi katika uendeshaji,” alisema Lumuli.

Awali akifungua Kongamano hilo, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Reli Kusini mwa Afrika, Siza Mzimela, ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli katika ukanda wa SADC kuchukua jukumu la kuboresha hali ya miundombinu kwa ufanisi zaidi.

“Umuhimu wa reli katika kusukuma gurudumu la maendeleo haupingiki, na endapo njia hii ya usafiri haitaboreshwa Afrika haitaweza kuona umuhimu wa reli katika ufanisi wa matumizi ya rasilimali zake na utajiri tuliojaaliwa,” alisema Mzimela.

Kupitia maonesho yanayoenda sambamba na kongamano hilo, Shirika la Reli Tanzania limeshiriki kuonesha juhudi na mikakati ya serikali katika kuleta mageuzi ya usafirishaji kwa njia ya Reli.

“Kupitia ushiriki wa TRC kwenye maonesho haya tumekutana na wenzetu kutoka nchi mbalimbali, kuanzia mashirika yanayotoa huduma kama za TRC mpaka kampuni zinazotengeneza vifaa vinavyotumika katika uendeshaji wa reli, kwa hiyo kwetu imekuwa ni fursa ya kukutana na wadau wapya, lakini pia kuona wenzetu wanafanya nini, au wao kujifunza kutoka kwetu,” alisema Mkuu wa Kitengo cha Habari, Jamila Mbarouk.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button