MATUKIO MAKUBWA YA MWAKA 2024: Treni ya SGR yainogesha Dar, Moro, Dodoma

MRADI mkubwa wa Reli ya Kisasa (SGR) nchini Tanzania, ambao unalenga kuboresha usafiri wa abiria na mizigo, umeendelea na mafanikio makubwa baada ya uzinduzi rasmi wa huduma za treni za abiria kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Uzinduzi huu ulifanyika Agosti 1, 2024, katika Stesheni ya SGR mkoani Dodoma, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, alikiri kuwa mradi huu utafungua milango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Samia alisema kuwa serikali imewekeza kiasi cha dola za Marekani bilioni 10 (sawa na Shilingi trilioni 23.3) katika mradi wa reli ya kisasa, na kwamba ujenzi wa reli hiyo umefanyika kwa kiwango cha kimataifa.
Alieleza kuwa reli hii itaongeza ajira, kupunguza msongamano wa magari, na kuboresha ufanisi wa bandari kwa kubeba mizigo mingi kwa wakati mmoja.
SOMA:RAIS DKT. SAMIA AKIZINDUA RASMI MRADI WA MKAKATI WA TRENI YA UMEME SGR DAR ES SALAAM-DODOMA
Maendeleo ya Mradi wa SGR
Akiwa kwenye hafla ya uzinduzi, Rais Samia alisema kuwa mradi huu ni matokeo ya juhudi za viongozi wa Tanzania katika awamu mbalimbali za utawala.
Alisema kwamba mradi wa SGR ulianza kwa mazungumzo ya viongozi wa Afrika Mashariki katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa, na kwamba ujenzi wake umeendelea chini ya Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete, Rais wa Awamu ya Tano Dk. John Magufuli, na sasa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dk Samia inaendeleza mradi huu kwa falsafa ya “kazi iendelee.”
“Reli hii ni faida kwa wananchi na kwa taifa zima. Itasaidia katika kuboresha uchumi, kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza kasi ya maendeleo,” alisema Rais Samia.
Majina ya Stesheni za SGR
Katika hatua nyingine, Rais Samia alikubali ombi la Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, na kuidhinisha kubadili majina ya stesheni za SGR.
Stesheni ya Dodoma itaitwa Samia Suluhu Hassan, Morogoro itaitwa Jakaya Kikwete, Dar es Salaam itaitwa John Magufuli, Tabora itaitwa Ali Hassan Mwinyi, Shinyanga itaitwa Abed Karume, Mwanza itaitwa Julius Nyerere, na Kigoma itaitwa Benjamin Mkapa.
SGR Inavyoboresha Uchumi
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema kuwa Tanzania imefanikiwa kumaliza ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa kwa kilometa 722, na kwamba nchi sasa inajivunia kuwa na reli ya SGR inayotumia nishati ya umeme.
Alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita inaendelea na ujenzi wa vipande vingine vya reli, hivyo kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kiongozi katika usafiri wa reli barani Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, alieleza kuwa shirika limewekeza kiasi cha Shilingi trilioni 1.8 katika ununuzi wa vichwa vya treni, mabehewa na treni za kisasa za EMU.
Treni ya EMU Yazinduliwa
Katika hatua nyingine, Shirika la Reli Tanzania limezindua rasmi treni ya Electric Multiple Unit (EMU) maarufu kama treni ya mchongoko, inayosafirisha abiria kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma.
Treni hii ina uwezo wa kubeba abiria 589, na safari yake ya kwanza ilifanyika Novemba 1, 2024. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alieleza kuwa mkoa wa Dodoma umeona mabadiliko makubwa, huku wakazi wakifaidika na ongezeko la mapato kupitia treni za SGR.
“Treni hizi zimeleta tija kwa wananchi. Kwa sasa tunashuhudia mabadiliko makubwa katika huduma za usafirishaji,” alisema Rosemary.
TRC na huduma bora
Kadogosa aliongeza kuwa TRC inaendelea kutoa huduma bora kwa abiria na kuanzisha mfumo wa kisasa wa ukataji tiketi kwa njia ya mtandao, ili kuhakikisha urahisi kwa abiria.
Alisema kuwa kwa sasa, TRC inasafirisha abiria zaidi ya 9,000 kwa siku, huku usafiri wa treni ukiendelea kuwa na umaarufu mkubwa.
Mradi wa SGR umeendelea kuwa alama ya mafanikio ya Tanzania katika kuboresha miundombinu ya usafiri, na ufanisi wake unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa taifa.



