Tril 1.3/-kutatua changamoto bonde mto Msimbazi

DAR ES SALAAM: SERIKALI imetoa kiasi cha Sh trilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa miradi itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo kwenye bonde la mto msimbazi katika Wilaya ya Kinondoni Dar es salaam.
Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Abbas Tarimba ameeleza hayo leo Aprili 29 wakati akizungumzia utekelezaji wa ilani uliofanyika jimboni humo katika viwanja vya Mwananyama kwa Kopa Wilaya ya Kinondoni katika ziara ya siku tatu ya Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla katika mkoa wa Dar es salaam.
Aidha, Makalla amepongeza jitihada zinazofanywa na Mbunge huyo kuhakikisha ufuatiliaji wa changamoto zinazowakabili wananchi wake na kuhakikisha zinafanyiwa ufumbuzi ili kuendelea kujenga imani ya wananchi juu ya CCM.
“Mimi nilikuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa ananisumbua sana kuhusu mradi ule wa mto Ng’ombe ni mfuatiliaji na mimi nilijitahidi pia alinileta mtaa wa fedha ambako kuna kituo kizuri cha afya na shule nzuri ya sekondari iliyojengwa bloku 41 Morocco,” amesema Makalla.
Akizungumzia jitihada za utekelezaji wa ilani zilizofanyika Tarimba alishukuru kazi kubwa iliyofanywa na Makalla akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa kusaidia utatuzi wa changamoto ya Mto Ng’ombe ambayo ilikuwa kero kubwa kwa wananchi wa Kinondoni.
Pia amesema changamoto nyingine inayowakabiri wannachi wa Kinondoni ni tatizo la mafuriko yatokanayo na bonde la Mto Msimbazi lakini serikali kwa kulitambua hilo na kuhakikihsa changamoto inatatuliwa imetoa kiasi tajwa cha fedha ili kujenga miradi itakayo saidia utatuzi wa changamoto hiyo.
“Tuna matatizo ya mafuriko bonde la mto Msimbazi mpelekee salamu mama Samia Wananchi wa Kinondoni tunadeni kwa sababu ametuletea Sh trilioni 1.3 kwa miradi ya kwenda kuondoa matatizo katika bonde la mto Msimbazi na hivi ninavyozungumza watu wameshalipwa fidia,” amesema Tarimba.
Ameongeza kuna ujenzi wa madaraja mengine matatu ambayo wakandarasi wapo wanaendelea ujenzi likiwemo daraja la Jangwani ambalo mkandarasi yupo ili kuondoa matatizo ya wananchi wa Magomeni.