ANGOLA : RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame wanatarajiwa kukutana Jumapili nchini Angola.
Mkutano huo ni awamu mpya ya mazungumzo yanayodhamiria kuumaliza mzozo wa Mashariki mwa Congo.
Mpaka sasa, Rwanda imethibitisha ushiriki wa Rais Paul Kagame atakayeambatana na Waziri wake wa Mambo ya Nje Olivier Nduhungirehe.
Kwa upande wake Rais Felix Tshisekedi amekubali kuhudhuria mazungumzo hayo licha ya kukataa hapo awali kuzungumza na Rwanda. SOMA: Kitengo kusitisha vita Congo kimezinduliwa
Mwenyeji wa mazungumzo hayo ya amani, Rais wa Angola Joao Lourenco, aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa msuluhishi amesema ana matumaini makubwa mazungumzo yatakayofanyika mjini Luanda yatawezesha kufikiwa makubaliano ya amani ya kudumu kati ya Congo na Rwanda.
Hivi karibuni, Rwanda na DRC zilitia saini nyaraka muhimu kwa ajili ya kuendeleza mchakato huo wa amani mashariki mwa Congo, eneo ambalo linalokumbwa na uasi wa makundi kadhaa yenye silaha.