TSN yatangaza neema kwa waandishi wa habari

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) inatarajia kutoa ajira kwa vijana hasa katika tasnia ya habari, mara baada ya kukamilika kwa mradi wa jengo jipya na mtambo wa uchapishaji magazeti Julai mwaka huu katika makao makuu ya kampuni hiyo Tazara, Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Machi 15, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Husna Sekibobo, baada ya kukagua mitambo na miradi ya ujenzi wa kiwanda cha kuchapisha magazeti, na  kujiridhisha kuwa maendeleo ya miradi hiyo ni mazuri na itaongeza fursa za ajira kwa vijana.

“Miradi hii italeta ajira kwa vijana hasa kwenye nyanja ya habari, kwani ofisi zinazojengwa zitahitaji wafanyakazi, na mitambo yote hii itahitaji wataalamu wa kuiendesha. Hivyo, miradi hii itazalisha ajira,” amesema Husna.

Pia, ameongeza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kupatikana kwa habari za uhakika, hasa kwa upande wa magazeti. Ameeleza kuwa magazeti yanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu na kuwa nyaraka muhimu, hasa magazeti ya Serikali.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hicho, TSN itakuwa na uwezo wa kuchapisha magazeti yake yenyewe. Aidha, itatoa huduma za uchapaji kwa watu, makampuni, na taasisi nyingine zitakazohitaji huduma hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji TSN, Asha Dachi ameeleza kuwa lengo la kamati hiyo kufika katika mradi huo ni kutathmini utekelezaji wake. Amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha mtiririko mzuri wa fedha ili mradi ukamilike kwa ufanisi, na kampuni iweze kujiendesha kwa faida.

Pamoja na hayo, ili mradi huo ukamilike kwa muda uliopangwa, kamati hiyo ya bunge imeisisitiza serikali kuhakikisha mtiririko wa fedha za mradi huo unaeleweka na fedha zinakuja kwa wakati.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button