CHANGAMOTO ya miundombinu hususani ya barabara na reli kutoka Mpanda kwenda eneo la Bandari ya Karema, iliyopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi imesababisha meli za mizigo kutotia nanga katika bandari hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Silaa, walipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa Ujenzi wa Bandari ya Karema, unaotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Akiongoza kamati hiyo Silaa amesema tokea ilipofunguliwa rasmi bandari hiyo Septemba 2022 hadi sasa, imeingiza kiasi cha Sh milioni 4.8, ambazo amesema ni kiasi kidogo ukilinganisha na uwekezaji uliofanyika wa Sh bilioni 47.97
“Tatizo kubwa la bandari ile ni barabara, mizigo kufika na kutoka pale, barabara na reli, iko reli ya kati unafika mpaka Mpanda na umbali wa kilomita 130 kufika mpaka Karema, ambazo hazijajengwa na wakati wote serikali imekuwa ikilisemea jambo hili,” amesema na kuongeza:
“Barabara tuliyoenda, kufika hata gari ndogo ni tabu, bandari ile inaweza ikapunguza msongamano Tunduma. Leo mizigo ya Congo malori yanatumia siku 45 maana yavuke Tunduma, yaingie Zambia, yaende tena yakavuke kweye mpaka mwingine wa Zambia ndio yanaingia Congo.”
Amesema kukamilika kwa miundombinu hiyo itasaidia malori yanayopeleka mizigo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), badala ya kupita njia ya Tunduma yatapita njia ya Mpanda na kwenda hadi Karema na baada ya kufika Bandari ya Karema ni rahisi kufika Bandari ya Karemii iliyopo DRC Jimbo la Lubumbashi.
Silaa amesema mpango wa serikali uliopo sasa ni kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kilomita 112, Kagwira hadi katika Bandari ya Karema pamoja na kujenga reli kutoka Mpanda hadi Karema.
Ameishauri serikali kuongeza kasi ya ujenzi na utunzaji wa miradi hiyo kwa kuwa bandari imekamilika kwa asilimia 100.
“Tunaamini barabara na reli au kimojawapo kikikamilika tutakuwa na uwezo wa kupeleka mizigo mikubwa inayokwenda Congo, inayotoka Bandari ya Dar es Salaam na mizigo inayotoka hapa Katavi kama ya chakula kwenda Congo na mizigo ya kutoka Congo ambayo inatumia Bandari ya Dar es Salaam basi itapita kwenye bandari ya Karema,” amesema.
Bandari ya Karema iliyopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ni kitovu cha biashara kati ya Tanzania na Congo kupitia ziwa Tanganyika kwenda Bandari ya Karemii iliyopo Congo.
Ujenzi wa Bandari ya Karema uligharimu kiasi cha Sh bilioni 47.97, ambapo ulianza kutekelezwa Oktoba 2019 na kukamilika Mei 2022 na kuanza kazi rasmi Septemba 2022.