Tuchape kazi zaidi kukuza uchumi

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo Juni 12 aliwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2025/2026.
Kwa ujumla, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Profesa Kitila, hali ya uchumi wa nchi kwa sasa ni himilivu, ukiwa na mwelekeo chanya na ukuaji endelevu.
Amesema kuimarika kwa uchumi kunatokana na usimamizi makini wa sera za uchumi jumla, pamoja na ushiriki wa wananchi wote katika ujenzi wa taifa.
Taarifa hiyo ya hali ya uchumi kwa mwaka 2024 inaonesha mafanikio kadhaa ikiwamo kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme kutoka megawati 2,138 zilizokuwepo Machi, 2024 hadi megawati 4,031.71 Aprili mwaka huu, na hivyo serikali imefikisha huduma ya umeme kwa vijiji vyote nchini.
Mafanikio mengine ni kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma, kukamilika kwa ujenzi wa daraja la kisasa la Kigongo – Busisi (JP Magufuli), ambapo kutachochea ukuaji wa uchumi, kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa zinazoingia nchini na zinazokwenda nchi jirani.
Kuongezeka kwa matumizi ya mbolea; kuongezeka kwa mchango wa viwanda katika ajira zote kutoka asilimia 8.1 mwaka 2023 hadi asilimia 12.8 mwaka 2024; kuongezeka kwa mchango wa bidhaa zilizozalishwa viwandani na kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini kutoka watalii 3,784,214 mwaka 2023/2024 hadi 4,244,266 mwaka 2024/2025.
Pia, kuimarisha kwa upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi kwa kujenga zahanati 980, vituo vya afya 367, hospitali mpya za halmashauri 129, hospitali tano za rufaa za mikoa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara pamoja na kukarabati hospitali kongwe 50 na kuboresha hospitali tisa za rufaa za mikoa.
Haya ni miongoni mwa mafanikio machache kati ya mengi yaliyopatikana kutokana na serikali kusimamia vizuri sera zake za uchumi na kuwezesha uchumi kukua na hivyo kuweza kutekeleza mipango ya maendeleo kikamilifu.
Hatua hii ya mafanikio ndio inayotupa faraja kuona Watanzania wakiendelea kufanya kazi kwa bidii, malengo ya Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2025/2026 yanayotarajiwa na serikali, yatafikiwa na pengine kuvuka malengo hayo.
Baadhi ya hayo ni kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa hadi kufikia asilimia 6.0, kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei, mapato ya ndani (mapato ya kodi na yasiyo ya kodi) kufikia asilimia 16.4 ya Pato la Taifa ifikapo 2025/2026 na mapato ya kodi kufikia asilimia 13.1 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2025/2026.
Kwa msingi huo, wito wetu Watanzania waendelee kuchapa kazi kwa bidii, walipe kodi kama inavyotakiwa na walinde na kutunza rasilimali za umma ambazo tayari zimejengwa kama vile miundombinu ya SGR, madaraja na barabara, ili kuvutia usafirishaji na uwekezaji wa ndani na nje ili kuongeza Pato la Taifa.