THOMAS Tuchel amethibitishwa kuwa kocha mpya wa kudumu wa England akilamba mkataba wa miezi 18.
Chama cha Soka England(FA) kimekuwa kikisaka mrithi wa Gareth Southgate tangu alipojiuzulu siku mbili baada ya taifa hilo kupokea kipigo toka Hispania katika fainali ya Kombe la Ulaya(UERO 2024) Julai mwaka huu.

Tuchel ataanza jukumu lake lenye thamani ya pauni milioni 6 kwa mwaka Januari 1, 2025 na anakuwa kocha wa tatu toka nje ya England baada ya Sven-Goran Eriksson na Fabio Capello.
SOMA: Thomas Tuchel akubali kuifundisha England
Katika taarifa iliyotolewa leo FA imethibitisha Tuchel amesaini mkataba Oktoba 15 na atasaidiwa na kocha wa zamani wa Chelsea na Bayern Munich, Anthony Barry.
Akizungumza baada ya uteuzi Tuchel amesema amekuwa uhusiano wa kibinafsi wa muda mrefu na soka la England na tayari umempa nyakati za kufurahisha.
“Ninajivunia sana kupewa heshima ya kuongoza timu ya England. Kuwa na nafasi ya kuiwakilisha England ni fursa kubwa, na nafasi ya kufanya kazi na kundi hili maalum na lenye vipaji la wachezaji ni ya kusisimua sana,” amesema Tuchel.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa FA Mark Bullingham amesema: “Tunafuraha sana kumwajiri Thomas Tuchel, mmoja wa makocha bora zaidi duniani, na Anthony Barry ambaye ni mmoja wa makocha bora wa Kiingereza kumsaidia. Mchakato wetu wa kuajiri umekuwa wa kina sana.”

Kocha wa muda Lee Carsley ataendelea kuiongoza timu ya wakubwa katika mechi za Nations League dhidi ya Ugiriki na Jamhuri ya Ireland mwezi ujao, kabla ya Tuchel kuiongoza England kuelekea fainali za Kombe la Dunia 2026 zilizopangwa kufanyika Marekani, Mexico na Canada.
Tuchel mwenye umri wa miaka 51 amezifundisha timu tano zikiwemo Chelsea, Borussia Dortmund, PSG na Bayern Munich.