Tujifunze maneno ya Dk Mpango mkutano wa AGRF na kuyatekeleza

JUKWAA la Mapinduzi ya Kijani barani Afrika la mwaka 2022 (AGRF 2022) linafanyika mjini Kigali, Rwanda na tayari wanazuoni na viongozi wamezungumza haja ya kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo barani humu.

Wamesema kwa nyakati tofauti kwamba kunahitajika mabadiliko makubwa katika uwekezaji na kukifanya kilimo kuleta utoshelevu wa chakula na pia kuwa cha kibiashara.

Miongoni mwa watu waliozungumza kwa ufasaha mkubwa katika mkutano huo ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ambaye aliyataka mataifa ya Afrika kuweka sera rafiki za kupata fedha za kuwavuta vijana na wanawake katika kilimo.

Makamu wa Rais, Dk Mpango alisema kama vijana watavutiwa na kujikita katika kilimo kutakuwepo na mabadiliko ambayo yataharakisha mabadiliko katika mfumo mzima wa kilimo, chakula na biashara.

Katika mkutano huo, Dk Mpango ambaye anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan akiwa amefuatana na viongozi kadhaa akiwemo Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wameonesha hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuimarisha sekta ya kilimo ili kuwa na uhakika wa chakula ikiwemo ajenda ya “10/30 kilimo ni biashara” inayolenga kukuza sekta hiyo kufikia asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030.

Ni dhahiri kama alivyosema Dk Mpango, Afrika kwa sasa hasa viongozi wa serikali na sekta binafsi kuwa mstari wa mbele kushiriki kwenye kilimo kwa kuwezesha vijana kujiingiza katika kilimo kwa kutengeneza sera rafiki za kilimo

Hakika ni sera hizo ambazo zitahamasisha vijana kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika kilimo kwa kuwa tayari watakuwa wamerahisishiwa utekelezaji wa mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo.

Tunasema hayo kwa kuwa tunaamini kuwa ni muhimu kwa viongozi kuangalia uendelezaji wa rasilimali watu kwani wao ndio watavumbua mazao mapya pamoja na kukuza teknolojia rafiki kulingana na mazingira husika.

Ili kuwa na kilimo na usalama wa chakula kwa nchi za Afrika hata hapa kwetu Tanzania tunatakiwa kutumia jukwaa hili kujifunza wenzetu wamefanya nini ili tuweze kuboresha pale tulipo na sisi kukifanya kilimo chetu kuwa cha uhakika na kinacholipa.

Na si jukwaa pekee lakini pia kama Watanzania tunahitaji kuyaangalia maneno ya Dk Mpango kwa Afrika kama jukumu letu kuonesha wenzetu kipi kinafaa kujitosheleza kwa chakula lakini pia kuwauzia wengine.

Maarifa aliyotoa Dk Mpango kwenye mkutano huo si siasa bali ni kauli thabiti yenye utaratibu unaostahili kuendelea kufanyiwa kazi ili tuweze kweli kuwa mfano kwa wengine.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button