Tukomeshe uchafuzi wa mazingira wa taka za plastiki

TANZANIA leo inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani inayoadhimishwa kila Juni 5, ikiwa ni uamuzi wa Mkutano wa Kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu masuala ya mazingira uliofanyika mwaka 1972 katika Mji wa Stockholm nchini Sweden.
Maadhimisho hayo yaliasisiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuelimisha wananchi kushiriki katika shughuli za hifadhi na usimamizi mazingira, kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira pamoja na kuhimiza matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira duniani.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya kimataifa ya siku hii ni, “Komesha Uchafuzi wa Mazingira Unaochangiwa na Taka za Plastiki.”
Kaulimbiu hii kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), inalenga kuhamasisha udhibiti wa taka zinazotokana na plastiki ambazo ni mojawapo ya changamoto kubwa ya uchafuzi wa mazingira ambao dunia inaendelea na jitihada za kutafuta ufumbuzi wake.
Kwa Tanzania, maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani yanafikia kilele leo katika Jiji la Dodoma na yameongozwa na kaulimbiu inayosema: “Mazingira Yetu na Tanzania ljayo Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki”.
Kaulimbiu hii imelenga kuikumbusha jamii ya Tanzania kuwa mazingira na rasilimali zake ni msingi wa uhai na maisha yetu pamoja na ukuaji wa uchumi. Hivyo utunzaji na uhifadhi wa mazingira na rasilimali zake ni jambo muhimu kwa kila mmoja wetu.
Hatua kadhaa zimechukuliwa na serikali katika suala la utunzaji wa mazingira na hasa eneo la plastiki ambako Aprili 9, 2019 serikali ilitoa tamko la kusitisha uzalishaji, uingizaji nchini, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kuanzia Juni Mosi, 2019.
Hatua hii imesaidia katika kudhibiti taka za plastiki na kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa kwani hatua za utekelezaji zimeonekana kwa kuboresha mazingira na pia jamii kuelewa umuhimu wa kutumia mifuko inayostahili kisheria na pia viwanda kuzalisha mifuko inayokubalika kisheria.
Kwa hiyo, kaulimbiu zote za maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Mazingira Duniani zimekuja wakati mwafaka kwa maana ya kukazia hatua ambazo zilishachukuliwa na mataifa mbalimbali ikiwamo Tanzania katika kudhibiti taka za plastiki.
Aidha, kaulimbiu hizi zimekuja wakati mwafaka kutokana na ukweli kuwa kwa sasa kuna dalili zimeanza kujitokeza nchini kwa baadhi ya wananchi na hata kampuni kutumia vifungashio vya plastiki ambavyo hazikubaliki kwa mujibu wa sheria ambavyo vimepigwa marufuku.
Vifungashio hivi vimekuwa vikitumika kama vibebeo vya bidhaa mbalimbali wakati havikidhi matakwa ya sheria mbalimbali na za mamlaka ya udhibiti ikiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Kwa msingi huu, tunaziomba mamlaka husika ziendelee kuchukua hatua kali kwa wote wanaohusika katika kuzalisha na kusambaza vifungashio hivi hatari kwa mazingira yetu.