Tulia aahidi ushirikiano wa Bunge, TSN

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson amekutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Tuma Abdallah.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwa Spika mjini Dodoma jana, Spika Tulia aliahidi Bunge kushirikiana na TSN katika kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inatekeleza majukumu yake ya kimsingi ya kuwa kiungo cha mawasiliano baina ya serikali na wananchi na kuelimisha umma kuhusu shughuli za Bunge.

Alisema serikali na bunge wanaelewa na kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na TSN katika utekelezaji wa majukumu yake na ndiyo maana mihimili hiyo imekuwa ikiunga mkono hatua hizo ikiwa ni pamoja na kutoa na kuidhinisha fedha nyingi ili kuiwezesha kutanua wigo wa utendaji wake.

Alisema pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya habari hivi sasa, TSN inao wajibu wa kuwekeza katika kujenga imani kwa jamii ili ifahamu kuwa ndiyo chombo cha kuaminika na kinachotoa taarifa sahihi kwa umma. “Nimesikia namna mnavyoendelea kutanua wigo wa huduma zenu. Niwahakikishie tu kuwa bunge lipo pamoja na ninyi katika kufikia malengo yenu.

“Pengine mnapoendelea kukamilisha uanzishaji wa huduma zenu mpya ikiwamo ya kiwanda kikubwa na cha kisasa cha uchapaji, ni vema kuwajulisha wabunge wote wajue kinachofanywa na TSN. Ni lazima wawafahamu zaidi pamoja na kwamba wanawafahamu,” alisema Spika.

Awali akielezea namna TSN inavyozidi kujitanua katika soko la habari nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Tuma alisema mwelekeo wa sasa ni kujikita katika magazeti mtandao na uchapaji wa kibiashara.

Kwa upande wa maendeleo ya uwekezaji katika kiwanda cha uchapaji wa kibiashara, Tuma alisema mpango mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinaanza uzalishaji Desemba mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao.

Alisema TSN imejitanua kwa kuanza kutoa huduma mbalimbali za kihabari ili kukabiliana na changamoto ya kuporomoka kwa soko la biashara ya magazeti na alizitaja baadhi ya huduma hizo kuwa ni kutoa ushauri wa kimedia, gazeti mtandao (E-paper), upigaji wa picha za kibiashara, maktaba kidijitali, machapisho ya elimu na majukwaa ya habari mtandao

Habari Zifananazo

Back to top button