Tulia ataka Waafrika wajiamini, wajisemee

KAMPALA, Uganda: RAIS wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesisitiza umuhimu wa Afrika na Waafrika kujiamini na kuzungumzia masuala yake yenyewe badala ya kusubiri watu wengine kuwazungumzia.

Dk Tulia alisisitiza hilo jana akiwashukuru maspika na wenyeviti wa mabunge wanachama wa Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika kwa kumuunga mkono na kumchagua kuwa Rais wa IPU kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba, mwaka jana nchini Angola.

“Mchakato ulikuwa mrefu na wa kuchosha, lakini tulifanikiwa kuvuka yote hayo pamoja kama Waafrika, kwa hiyo ningependa kutoa shukrani kwa juhudi kubwa mlizofanya katika kupambania nafasi hii,” alisema Dk Tulia.

Katika Mkutano wa 27 wa viongozi hao unaofanyika nchini Uganda, alisisitiza kuwa ushindi wake si ushindi wa Tanzania pekee, bali ni ushindi wa Afrika na dunia nzima, na aliwashukuru maspika kila mmoja kwa kuhamasisha wajumbe wake waliokuwa wanashiriki mkutano Angola kumchagua kwa kumpigia kura awe Rais wa IPU.

“Kwa hiyo nasimama mbele yenu kuwashukuru kwa kujiamini kwenu na kuniamini mimi, nawashukuru sana. Natamani ningekuwa na maneno bora zaidi ya kusema, lakini yako mawili ya kusema,” alisema.

Dk Tulia alisema kwanza angependa kusisitiza alichosisitiza wakati wa kampeni kuwa anataka kuitumikia dunia na kuifanya iwe sehemu salama, lakini pia atakuwa sauti ya masuala ya Afrika.

Alisema ni muhimu Afrika na Waafrika kujielezea wenyewe badala ya kutegemea wengine kuwazungumzia.

“Tuzungumze wenyewe na mimi kila nitakapopewa nafasi ya kuzungumza nitazungumza tunachofikiria Afrika, kile tunachofikiria ni sawa kwetu sisi na tutafanya hivyo kwa vitendo, kwa sababu watu wanaelewa vizuri kwa vitendo kuliko maneno… pale nitakapotakiwa kuchukua hatua, nitafanya hivyo kwa kupata mwongozo kutoka kwenu,” alifafanua.

Alisema anaposema atazungumza kwa kuongozwa na wanachama wa Afrika, ana maana ushindi aliopata ni kwa ajili ya Afrika, na sasa Mwafrika amekuwa Rais na Urais unamilikiwa na Afrika, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuwezesha na kufanikisha hilo.

“Kwa kweli nitategemea mwongozo na ushauri wenu. Sipo katika hili peke yangu na ndio maana tuliitafuta nafasi hii pamoja,” alieleza.

Dk Tulia alisema imefika wakati wa Afrika kukaa pamoja kama ndugu na kuwa Waafrika wanatakiwa kuungana na kutoa kauli moja, kujifunza na kufanya uamuzi utakaoheshimiwa na si jambo jema watu wengine kuwachagulia nani anafaa kuwaongoza.

Aliwaomba wajumbe wa Afrika kuonesha wana uwezo wa kuzungumza, wana uwezo wa kufanya uamuzi wao wakisimama kama kitu kimoja.

“Yapo mengi tumejifunza na mojawapo ni hili la Afrika kusimama kama umoja bila kujali wengine nje ya Afrika wanavyofikiri. Tukisimamia hili tutasonga mbele kwa haraka,” alisema Rais wa IPU.

Alisisitiza kama viongozi wa mabunge wanaweza kupeleka hoja kwenye serikali zao kwa sababu wabunge ni washauri wa serikali na kama Afrika anaamini wanaweza kufanya vizuri na makubwa duniani kutokana na idadi kubwa na takwimu zilivyo.

“Asanteni sana Mwenyekiti kwa nafasi ulionipa, natarajia kutembelea nchi kadhaa Afrika, labda sio nchi zote angalau hata kwa kanda zenu, basi mkisikia niko nchi jirani na ya kwako vukeni mipaka mje tukutane na kuifanya fursa hii ya Urais kuwa ya faida kwetu. Nawashukuru tena kwani najivunia kuwa Rais wa IPU kuwahudumia Afrika na dunia kwa jumla,” alisema Dk Tulia.

 

Habari Zifananazo

Back to top button