Tulia azidi kung’ara mbio Urais mabunge duniani

WABUNGE wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamempitisha Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson kugombea nafasi ya Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Uchaguzi wa IPU unatarajiwa kufanyika Oktoba 27, mwaka huu nchini Angola. Mbunge wa Bunge la Afrika ya Kusini, Darren Bergman ndiye aliwasilisha hoja katika bunge hilo katika kikao cha 53 cha Jukwaa la Mabunge ya SADC kinachoendelea jijini Arusha na kuomba mabunge yote kumuunga mkono Dk Tulia.

Alitoa hoja ya kupitishwa Dk Tulia kuwania nafasi hiyo, kwa mujibu kwa kanuni ya 26(4) ya utaratibu katika bunge hilo. Alisema amewasilisha hoja ya kupata mgombea mmoja kutoka SADC, licha ya kuwepo wagombea wengine walioonesha nia ya kugombea nafasi hiyo kutoka Afrika.

Wagombea hao ni Catherine Gotan Hara wa Malawi, Jacob Mudenda wa Zimbabwe na Adji Kanoutee kutoka Senegal. Bergman alisema ili kuonesha umoja katika kuwania nafasi hiyo ni vyema kumpitisha Dk Tulia, kutokana na sifa alizonazo kuwa mgombea wa SADC katika uchaguzi huo wa IPU.

Hoja ya Mbunge huyo wa Afrika Kusini, iliungwa mkono na mbunge kutoka Angola, Pedro Sebastiano na kueleza kwa kuwa muda mrefu nafasi hiyo imekuwa ikishikwa na wabunge wanaume.

Alisema kumpitisha Dk Tulia ambaye ni msomi na kijana kuwania nafasi hiyo kutawezesha ushindi kupatikana. Dk Tulia tayari amepitishwa pia na Bunge la Afrika (PAP) na Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EALA) kuwania nafasi hiyo.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button