Tulia: Tanzania Iko Tayari kwa IPU

TANZANIA imewahakikishia wajumbe na wageni watakaoshiriki Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuwa imeweka na kuimarisha hatua zote muhimu za usalama na afya kuelekea mkutano huo utakaofanyika Oktoba 5 hadi 9, 2026 jijini Arusha.
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amesema maandalizi ya Tanzania yanaendelea vizuri na kwamba mazingira yote muhimu kwa ajili ya kufanikisha mkutano huo yamezingatiwa.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wajumbe wa IPU katika mji mkuu wa Serbia, Belgrade, Dkt. Tulia alisema Tanzania ipo tayari kuwapokea washiriki kutoka mataifa mbalimbali watakaohudhuria mkutano huo wa kimataifa. “Tanzania iko tayari kwa Mkutano wa 153 wa IPU na tayari kila aina ya hatua za usalama, ikiwemo huduma za afya, zimezingatiwa,” alisema Dkt. Tulia.
Mkutano wa 153 wa IPU unatarajiwa kukutanisha wabunge, viongozi wa mabunge na wadau wa masuala ya demokrasia kutoka nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kujadili masuala ya maendeleo, amani na ushirikiano wa kimataifa.



