GLORIA Tibaijuka na Halima Muhunzi wenye umri wa miaka 16, ni wanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani.
Hawa ndio washindi wa jumla wa Tuzo za Wanasayansi Chipukizi (YST) kwa mwaka 2022. Hawa wanasayansi chipukizi wanaonesha umuhimu wa maji kwani wahenga walisema, “Maji ni uhai.” Vijana hawa wa kike ambao ni wanasayansi chipukizi wameshiriki utafiti kuhusu Bonde la Mto Ruvu unaosambaza maji katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Utafiti huo ulifanyika baada ya wanafunzi hao kugundua kwamba, shughuli za kibinadamu zinazoendelea pembezoni mwa bonde hilo husababisha upungufu wa maji, hivyo kuchangia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kushindwa kusambaza maji kadiri ya mahitaji.
Jopo la wanasayansi waliobobea kupitia Shirika la Wanasayansi Chipukizi (YST), walipitia utafiti huo na mapendekezo waliyoyatoa wanafunzi hao kwa serikali katika kulinda chanzo hicho na kutafuta vyanzo vingine vya maji.
Kutokana na utafiti na mapendekezo yake, Tibaijuka na Muhunzi wamekuwa washindi wa jumla wa tuzo za YST kwa mwaka 2022.
Katika tuzo hizo zilizotolewa Desemba 8, wanafunzi hao walitangazwa rasmi kuwa vinara wa YST na kupewa udhamini wa masomo yao ya Chuo Kikuu na Taasisi ya Karimjee Jivanjee (KJF) ili kuwafanya kuwa wanasayansi mahiri watakaoisaidia Tanzania kutoa majawabu ya changamoto zinazoikabili jamii.
Akielezea kuhusu mradi huo, Muhunzi anasema Bonde la Mto Ruvu ni miongoni mwa mabonde makubwa Afrika Mashariki. Lina urefu wa kilometa 18,000. Maeneo ya Mgeta, Ngerengere hukusanya maji na kumwaga katika mto huo ambao ni tegemeo kwa usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
“Bonde la Mto Ruvu hutegemewa kwa asilimia kubwa na wakazi wa Dar es Salaam, Kibaha na maeneo kadhaa ya Morogoro Mjini. Matumizi makubwa ya mto huu ni katika viwanda, mahitaji ya nyumbani na kilimo cha umwagiliaji,” anasema Muhunzi.
Anasema kutokana na umuhimu wa mto huo, walifikiria hali iliyopo sasa na itakavyokuwa baadaye kwa maana ya mahitaji ya ubora na ujazo wa maji.
“Lengo la mradi huu tulioufanyia utafiti lilikuwa kuangalia ustahimilifu wa kituo cha kusukuma maji cha Ruvu kinachopatikana katika Bonde la Mto Ruvu ili kukidhi mahitaji ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam katika nyanja zote,” anasema.
Mradi huo uliangalia mahitaji yaliyopo sasa na sababu zinazoweza kuathiri upatikanaji na usambazaji wa kiwango tarajiwa cha maji katika bonde ili kuhakikisha unaenda sambamba na ongezeko la idadi ya watu na maendeleo ya kiuchumi kwa miaka ijayo.
Anasema njia walizotumia kukusanya taarifa ni kuandaa maswali ya dodoso ambayo wanafunzi wenzao wa Kibaha na Shule ya Sekondari Ruvu walishiriki kuyajibu baada ya kutembelea mto huo.
Aidha, walitembelea Dawasa ili kupata taarifa za makusanyo ya maji kwa mwaka na usambazaji kwa miaka mitano, kufanya mahojiano na wafanyakazi waliopo kwenye Kituo cha Ruvu, wakulima waliopo pembezoni mwa mto na maofisa wa kilimo.
Kwa upande wa Tibaijuka, anasema katika mradi huo walibaini ongezeko kubwa la watu katika mikoa hiyo na inayotegemea maji kutoka Mto Ruvu.
Anasema mwaka 2025 idadi ya watu watakaokuwa wanategemea mto huo utakuwa zaidi ya asilimia 63.
8. “Kwa mwaka 2020, mahitaji ya maji katika kila sekta ilikuwa mita za ujazo 410,568,487 kwa mwaka na Dawasa imesambaza maji yenye mita za ujazo 155,515,724 kutoka Mto Ruvu na kwenye vyanzo vingine imefanya wastani wa usambazaji wa maji kuwa mita za ujazo 255,052,763 kwa mwaka sawa na upungufu wa asilimia 62.1,” anasema Tibaijuka.
Anasema matokeo hayo yanaonesha kuwa, mahitaji ya maji yanaongezeka katika kila mkoa huku kwa asilimia kubwa wakitegemea mto huo kwenye uzalishaji. Mwanafunzi huyo anasema mahitaji ya maji yataongezeka kwa asilimia 43.4 ifikapo mwaka 2025 kutoka mita za ujazo 284,453,463 mwaka 2011 hadi mita za ujazo 502,213,380 mwaka 2025.
Anasema uzalishaji na usambazaji wa maji kwa Dawasa utaongezeka kutoka asilimia 7.3 hadi asilimia 11.6. “Tofauti hii kati ya mahitaji na usambazaji wa maji itaathiri moja kwa moja shughuli za kiuchumi na kijamii endapo tutaendelea kutumia Mto Ruvu pekee kama chanzo cha maji,” anasisitiza.
Tibaijuka anaongeza kuwa: “Nimefurahi sana kushinda tuzo hii kwa sababu ni kitu kilichonipa matumaini kwamba nitashinda. Tatizo lililopo kwenye mto huu ni kwamba shughuli za kiuchumi ikiwemo za viwandani, matumizi ya nishati na kilimo husababisha uharibifu wa mto huu.” Akiwa mwanasayansi chipukizi amewahamasisha wanafunzi wengine wa kike kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kubuni mawazo mbalimbali ya kisayansi kwani YST inaangalia mawazo yanayolenga kutatua matatizo kwenye jamii.
Akieleza zaidi kuhusu mradi huo, Muhunzi anasema ukosefu wa maji uliwahi kutokea mwaka 2020 kwa sababu ya kushuka kwa kiwango cha maji katika mto huo.
“Dawasa haiwezi kusambaza maji katika mikoa hii miaka mitano inayokuja endapo jamii husika itaendelea kutumia chanzo hiki pekee, Tanzania kuna vyanzo vingi vya maji hivyo vitumike kusambaza maji,” anasema Muhunzi.
Kwa mujibu wa Muhunzi, ni wakati wa kutoa elimu kwa watu wanaojihusisha na shughuli mbalimbali pembezoni mwa mto huu ili waelewe namna ya kutunza chanzo hiki kwa kupanda miti kusaidia utengenezaji wa mvua.
Anasema wameishauri serikali kutafuta chanzo cha kudumu cha maji ili kusambaza maji katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee kwa sababu kuna watu wengi, shughuli nyingi za kiuchumi na viwanda, hivyo kutumia mto huo pekee hakutaleta mafanikio tarajiwa.
“Tumeshauri Mto Ruvu utumike kusambaza maji katika mikoa ya Pwani na Morogoro, pia kujengwe visima vikubwa kwa ajili ya kuhifadhia maji na wakulima watumie njia za kisasa za kuhifadhi maji kwa ajili ya kilimo,” anasisitiza.
Mtafiti huyo chipukizi anafafanua kuwa, walipotembelea mto huo walibaini kuwapo watu wanaokata miti kwa ajili ya kuni na mkaa, ulishaji wa mifugo pembezoni mwa mto na kuna kiwanda karibu na mto ambacho kimeruhusiwa kufanya kazi na taasisi ya NEMC.
Hata hivyo, anasema watoto wa kike wana vitu vingi wanavyoshindwa kufanya kutokana na hofu, hivyo anawashauri wajiamini kwani wasichana pia wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi.
Anasema baada ya kumaliza elimu yake anapenda kuwa daktari wa upasuaji na kuwa kiongozi ambaye atatatua changamoto za wanajamii. Mwalimu wa wanafunzi hao, Paul Balibate, anasema walibuni wazo lao wenyewe na kufanya utafiti wa kisayansi kama walivyowaelekeza hatua za kufuata kufanya miradi hiyo ikiwemo walichogundua na wanachoshauri kama wanasayansi chipukizi.
Anasema walikuwepo wanafunzi wengi waliokuwa na mawazo mbalimbali na kutumwa YST na wazo hilo pekee kutoka shuleni hapo ndio lililopita na walifanya vizuri na kushinda.
“Kama kiongozi wao na mratibu wa YST Mkoa wa Pwani, nimefurahia ushindi wa wanafunzi hawa; inanitia moyo kuendeleza kazi yangu.
“ “Tunaendelea kushauri wanafunzi wa kike kuwa katika mashindano haya kwa sababu hata watoto wenyewe wanaweza kubuni mawazo wao,” anasema Mwalimu Balibate.
Anasema YST inawapa wanafunzi uwezo wa kutafuta changamoto na kuzitatua hivyo wanatengeneza watafiti wengi ndani ya nchi kwa maendeleo.