TUME ya Waziri Mkuu ya kukusanya maoni kuhusu changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini imewafikia wafanyabisahara wa Mkoa wa Kigoma ambao wametoa maoni yao wakieleza kero kubwa ya tozo na kodi kwa bidhaa na biashara wanayofanya ya kuvuka mpaka.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma wafanyabiashara hao wameinyooshia kidole Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wakitaka ifanye kazi zake kwa kusimamia kodi na tozo ambazo ni rafiki kwa wafanyabiashara.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Brian William Wakala wa forodha katika Bandari ya Kigoma alisema kuwa utitiri wa kodi na tozo umekuwa changamoto kubwa kwao kwani kodi ya upakiaji na upakuaji wa shehena imekuwa kubwa kwa bandari hiyo ukilinganisha bei ya chini kwa Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema kuwa hali hiyo imefanya wafanyabiashara wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kusafirishia shehena zao kupitia Bandari ya Mpulungu Zambia ambayo inatoka Dola 65 kwa kontena ukilinganisha na dola 140 Kigoma.
Naye Mfanyabiashara wa gesi, Issa Mangapi alisema kuwa kodi na Tozo za TRA na manispaa zimekuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara ikiwemo kodi ya huduma (Service Levy) ambayo ametaka iondolewe huku akiitaka serikali itumie wataalam wake kufanya utafiti wa kodi na tozo ambazo ni kero kwa wafanyabiashara.
Francis Kabula Mwenyekiti wa wavuvi katika Ziwa Tanganyika ameitaka serikali kuangalia kodi na tozo zinazotozwa TASAC kwenye maboti ya usafirishaji mizigo na abiria na mitumbwi ya uvuvi kwani haziendani na mapato yanayopatikana kwenye maboti yao.
Akizungumza kabla ya kuhitimisha kikao hicho Mjumbe wa Kamati ya Waziri Mkuu ya kukusanya maoni kuhusu kero za wafanyabiashara, Rehema Madenge alisema kuwa maoni hayo yaliyotolewa na wafanyabiashara yatawasilishwa kwa Waziri Mkuu kama maelekezo yalivyotolewa.
Madenge ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa Dar es Salaam amewataka wafanyabiashara kutoa maoni na kero zao ili ziweze kufanyiwa kazi kuwezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa tija na kuondoa kero zinazowakabili.