Tume yaomba ushirikiano uwajibikaji viongozi wa umma

DAR ES SALAAM: TUME ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka wahariri na waandishi wa habari kuendelea kushirikiana nayo katika kuwaibua viongozi wanaokiuka maadili, ili kuimarisha uwajibikaji na utawala bora nchini.

Akizungumza leo Mei 30, 2025 katika kikao cha wahariri kilichoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili, Kamishna wa Maadili, Jaji Sivangilwa Mwangesi, amesema malalamiko mengi kutoka kwa wananchi yamekuwa yakihusisha matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa maadili na hivyo Tume imeanzisha mfumo rasmi wa kupokea malalamiko kutoka kwa umma.

“Majukumu ya Tume ni kupokea na kuchunguza malalamiko dhidi ya viongozi wanaokiuka maadili. Wananchi wanahimizwa kuripoti viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kutumia mifumo rasmi ya Sekretarieti,” amesema Jaji Mwangesi.

SOMA ZAIDI

Tume kukamilisha sheria makosa ya maadili

Ameongeza kuwa tume imeandaa semina kwa wahariri na waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuelimisha jamii kuhusu maadili ya viongozi wa umma.

“Wahariri wanatakiwa kutumia ubunifu na kalamu zao kulinda maadili ya viongozi kwa kuwaibua wale wanaokiuka taratibu,” amesema.

Katika kikao hicho, kamishna pia amekumbusha kuwa kila kiongozi wa umma anatakiwa kujaza tamko la rasilimali na madeni, na kwamba kutotekeleza wajibu huo ni kosa la kisheria.

“Kiongozi asipojaza tamko bila sababu ya msingi anapelekwa kwenye Baraza la Maadili ambalo hufanya kazi kama mahakama ya watumishi,” amefafanua.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria na Maadili, Emma Gelani, amesema kuwa viongozi wanaokiuka maadili huchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, kushushwa cheo au kusimamishwa kazi, kulingana na uzito wa kosa.

“Viongozi wanaotumia madaraka vibaya, wanaopendelea katika maamuzi, au wanaotumia mali ya umma kwa maslahi binafsi, wote hukabiliwa na hatua kali za kinidhamu,” amesema Gelani.

Aidha, alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya viongozi 10 walichukuliwa hatua mbalimbali kwa makosa ya ukiukaji wa maadili ya viongozi wa umma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button