RAIS Samia Suluhu Hassan amesema taifa linajivunia yale yaliyofanywa na hayati Edward Lowassa enzi za uhai wake na utumishi wake serikalini.
Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati aliposhiriki maziko ya hayati Lowassa yaliyofanyika kijijini kwake Ngarashi wilayani Monduli mkoani Arusha leo.
Mkuu huyo wa nchi amesema Lowassa alipenda vijana wapate ujuzi na maarifa ndio maana alipokuwa mgombea urais mwaka 2015 aliweka wazi kipaumbele chake cha kwanza kuwa ni elimu na pili elimu na cha tatu elimu.
“Lowassa alikuwa muumini wa elimu kama nyenzo ya kujikwamua na umasikini na mara zote alisistiza kwamba haupendi umasikini,”
“Ninakumbuka aliwahi kusema nimekuwa na nitaendelea kusisitiza umuhimu wa elimu bora kwa wote, elimu inayowaandaa vijana kuingia kwenye soko la ajira la dunia”. amesema
Ameongeza kuwa dhamira ya Lowassa ya kutaka kusimamia sekta ya elimu ndio matunda yanayoonekana sasa ya kuimarika kwa sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ongezeko kubwa la shule nchini.