Tunapongeza Mahakama kuiheshimisha nchi

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro.

TANZANIA imezidi kung’ara katika sekta mbalimbali Afrika, ikiwemo ya mahakama.

Imeelezwa kwamba utendaji wa mahakama nchini umepiga hatua kubwa katika kusimamia mashauri na kutoa haki kwa wakati katika Afrika, jambo linalozifanya nchi nyingi kuomba kuja nchini kujifunza namna ya uendeshaji wa mashauri.

Hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro alipokuwa akifungua Wiki ya Sheria mkoani Kigoma.

Advertisement

Dk Ndumbaro alisema sifa kwa Tanzania, zilitolewa katika kikao cha mawaziri wa sheria wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia, makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU), ambacho naye alihudhuria.

Ikiwa mawaziri wa sheria Afrika wameona na kupongeza utendaji kazi wa mahakama za Tanzania na mafanikio yake, ni jambo linaloongeza ari ya bidii katika utendaji huo ili kutopoteza sifa hizo njema kwa taifa katika jicho la kitaifa na kimataifa.

Katika mkutano huo, Waziri wa Sheria wa Morocco aliwaeleza viongozi wenzake kuwa nchi hiyo ilifanya utafiti wa uendeshaji kesi katika nchi za Afrika na kuona Tanzania inashika namba moja kwa kuwa na uendeshaji bora wa shughuli za mahakama.

Tunaamini sifa hizi si ndogo, bali Watanzania wana kila sababu ya kujivunia juhudi kubwa za uboreshaji wa mahakama zilizofanywa na kuongeza utendaji wa kidijiti katika uendeshaji wa mashauri, ujenzi wa miundombinu ya mahakama kuanzia ngazi ya mwanzo mpaka mahakama kuu.

Kwa mfano, waziri huyo wa Morocco kwa mujibu wa Dk Ndumbaro, alisema jambo kubwa ambalo linaipa Tanzania heshima hiyo ni uboreshaji mkubwa wa mfumo wa mahakama uliofanyika ambao mambo mengi yamerahisishwa, kuboreshwa na kuifanya mahakama kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Huu ni ukweli mtupu kwamba kazi kubwa ya kuboresha mahakama imefanyika nchini. Tunaipongeza serikali na mahakama kwa ujumla kwani inaendelea kuifanya nchi kung’ara kimataifa.

Uboreshaji huu wa mifumo, majengo na utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania umeifanya mahakama kutekeleza majukumu yake kwa tija na kutimiza malengo ya dira ya taifa ya uboreshwaji wa shughuli za mahakama katika kusimamia utoaji haki.

Tunatoa pongezi za dhati kwa Mahakama kwa kuiheshimisha nchi huku tukiisihi iendelee na utendaji uliotukuka nchi izidi kupaa si tu katika Afrika bali duniani kwa ujumla.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *