Tuungane pamoja katika kukemea, kutokomeza udhalilishaji, unyanyasaji
TUNAISHI wakati ambao ni tete pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya kuwapo kwa ulimwengu.
Ninasema hivyo kwa sababu, kila uchao takwimu za matukio ya udhalilishaji, vitisho na mauaji zinaongezeka.
Kwa mfano, huko visiwani Zanzibar, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Watoto (UNICEF), asilimia 64 miongoni mwa kesi za udhalilishaji, ni udhalilishaji wa kingono kwa watoto visiwani humo.
Matukio ya udhalilishaji, kama kubaka na kulawiti, kuwakumba idadi kubwa ya watoto, wa kike kwa wa kiume.
Kwa mujibu wa utafiti wa shirika la Unicef, mtoto mmoja kati ya 10 wa kiume hukumbana na udhalilishaji wa kingono, na mmoja kati ya watoto wa kike 20 naye hukumbana na udhalilishaji wa kingono.
Kwa mawazo yangu ipo haja kila mmoja wetu popote alipo kukemea mambo hayo ili kuhakikisha jamii yetu hasa watoto wanaishi katika mazingira salama, wezeshi na rafiki ili watoto hao watimize ndoto zao maishani.
Suala la udhalilishaji na unyanyasaji wa waoto si Zanzibar pekee bali ni maeneo mengine nchini kunaripotiwa matukio ya mauaji na mambo yanayofanana na hayo. Mkoani Songwe, kulitokea mauaji ya watu wawili wa familia moja kwa kile ilichoelezwa kwamba ni kulipizana kisasi.
Matukio haya na mengine yananifikirisha na kunitafakarisha kwamba, hatuna budi kumwomba Mungu atusaidie kuwa watu waungwana na wenye upendo kwa ajili ya jamii yetu baina yetu sisi kwa sisi ili dunia iwe mahala bora zaidi pa kuishi.
Ukiachilia mbali namna wanadamu tunavyoishi sisi kwa sisi, tunashuhudia hali mbaya ya hali ya hewa kwa maana ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Hali hiyo imechangia pakubwa mataifa mengi duniani kuwa na upungufu wa chakula hali inayoendelea kutishia usalama wa chakula na maisha ya utangamano kwa ujumla.
Natoa shime kwa kila mmoja kwa dini yake tupige goti tumwombe Mungu aingilie kati apunguze matatizo yanayoisibu dunia kwa sasa na siku za usoni ili tuendelee kuishi kwa jicho na siha yake Mwenyezi Mungu.
Pamoja na juhudi na umuhimu wa vyombo vya dola na wataalamu wa masuala ya mazingira, bado dua na sala kutoka kwa Mungu ni muhimu na itaendelea kuwa jawabu lenye uhakika katika kuleta suluhu ya hali tete zilizopo.