“Tuwe wabunifu, tutatue changamoto”

SERIKALI imeihakikishia Kampuni ya Magazeti Tanzania (TSN) kuendelea kuipa ushirikiano ili iendelee kuisemea kupitia kuwahabarisha Watanzania taarifa mbalimbali zikiwemo za kimaendeleo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Methusela Ntoba amesema hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Palamagamba Kabudi kwenye ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa TSN uliofanyika Dar es Salaam.

Advertisement

‘’Nafahamu kunaweza kuwa na changamoto mbalimbali zinazowakabali, njia pekee ya kuzikabili changamoto ni kuzigeuza kuwa fursa na siyo kuleta malalamiko hayatoi suluhisho bali yanakuza tatizo na kukwamisha jitihada za utatuzi, tuwe wabunifu tutatue changamoto,’’amesema Ntoba.

Ameongeza kuwa “Sote tunafahamu kuwa TSN ni chombo muhimu cha serikali kwani ni chombo cha mawasiliano kati ya wananchi na serikali yao. Suala la mawasiliano ni suala muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wanahitaji uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya nchi yetu,’’.

‘’Tukiwa watendaji wa TSN, tuwajibike, tufanye kazi kwa bidii na weledi, tusingatie maadili ya utumishi wa umma ikiwemo miiko ya taaluma zetu. Sisi katika sekta hii ya mawasiliano tuwe mfano wa kuigwa na tuimarishe ushirikiano miongoni mwetu, tusikubali kufanya kazi kwa matabaka na tuheshimiane, tuthaminiane katika kutimiza malengo ya taasisi ,’’amesema

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi TSN, Asha Dachi amesema kikao hicho ni sehemu ya kujadili fursa mbalimbali na kuwawezesha wafanyakazi wa TSN kufanya kazi vizuri.

‘’Kikao hiki kinawapa fursa wafanyakazi kutoa maoni ya mpango wa bajeti na ushirikishwaji. Tunajua kuwa tuna changamoto ya rasilimali kwa upande wa vitendea kazi ambavyo vinasaidia kuinua mapato pamoja na changamoto ya upatikanaji fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kiwanda. Ombi letu kwa serikali kutupia macho kwenye suala hili kwa sababu tunachapa magazeti kwa kutumia gharama kubwa,’’amesema Dachi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TSN, IGP Mstaafu, Said Mwema amewataka wajumbe wa baraza hilo kujadiliana kwa kutumia 4R za Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo kufanya maridhiano ya mpango kazi wa bajeti ya taasisi ya 2025/2026 ili TSN itoke sehemu moja hadi nyingine.