Tuzo Chaguo la Wateja kufanyika Novemba

DAR ES SALAAM; TUZO za Chaguo la Wateja (CCAA) zinatarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo, mwandaaji na Mkurugenzi wa CCAA, Diana Laizer amesema mwaka huu zitakuwa tofauti na miaka mingine na kwamba wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Afrika Kusini, Kenya, Malawi, Nigeria na wenyeji Tanzania wanatarajiwa kuteua chapa zao.

“Tukio la mwaka jana lilikuwa na vipengele vikuu 22 na jamii 70 katika mkutano huo. Vipengele hivyo vilijumuisha vifaa, mawasiliano ya simu, usafiri wa anga, huduma za kifedha, mali isiyohamishika, bima, mafuta na gesi, hoteli na ukarimu, usalama, bidhaa za walaji zinazokwenda kwa kasi, matukio na mapambo, mitindo na muundo, na upigaji picha,” amesema Laizer.

Amesema anatarajia tuzo hizo zitaongeza ushindani na kuwapa motisha wajasiriamali, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

“Tangu kuanzishwa kwa tuzo hizi tumeona mafanikio makubwa ambapo jumla ya washiriki 650 wa tuzo hizo za mwaka jana, ni wanufaika,” amesema Laizer na kueleza kuwa wanatarajia kuwa na mfumo mzuri na kwamba washindi watachaguliwa kwa kuzingatia vigezo na ubora wa bidhaa zao.

“Kenya tayari wameshashikilia tuzo zao za kitaifa tangu Machi mwaka huu, huku Malawi wakitarajiwa kutangaza washindi wao hivi karibuni, pamoja na nchi nyingine. Mwitikio huu unaonesha jinsi tuzo hizi zinavyoendelea kukua,” amesema.

Akifafanua mchakato wa uteuzi huo, amesema washindi wa kategoria mbalimbali hupatikana kupitia uteuzi wa mtandaoni.

“Baada ya kupokea mapendekezo ya washiriki katika kategoria tofauti, timu yetu inafanya kazi ndani katika kupanga majina na kategoria na kutathmini kila pendekezo lililotolewa kwa kurejelea vigezo vya kila tuzo. Tarehe rasmi ya tukio itajulishwa baadaye,” amesema Laizer.

Habari Zifananazo

Back to top button