Twiga Stars yajiweka sawa kuivaa DR Congo

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Bakari Shime, amesema kikosi chake kimejiandaa ipasavyo kuelekea mchezo wa kirafiki dhidi ya DR Congo utakaopigwa leo saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu, Shime amesema licha ya baadhi ya wachezaji kujiunga na kambi kwa mafungu kutokana na majukumu ya klabu zao, kambi ya wiki mbili imekuwa na mafanikio makubwa.
“Tumekuwa na kambi ya wiki mbili. Ingawa wachezaji waliingia kwa mafungu kambini, asilimia kubwa tayari wameripoti, isipokuwa mmoja ambaye tunatarajia atajiunga muda wowote,” alisema Shime.
SOMA ZAIDI
Kocha huyo amesema mchezo wa leo pamoja na ule wa marudiano utakaochezwa Juni 3, ni sehemu muhimu ya maandalizi kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) zitakazofanyika Julai mwaka huu nchini Morocco.
“Kimbinu tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata matokeo mazuri. Lengo letu ni kutumia michezo hii miwili kama sehemu ya kujiangalia wapi tupo kuelekea mashindano ya WAFCON,” aliongeza.
Aidha, Shime alieleza kuwa uwepo wa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi ni faida kubwa kwa kikosi hicho, akisema uzoefu wao unatarajiwa kuimarisha viwango vya timu kwa ujumla.
Twiga Stars wanatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya DR Congo ikiwa ni sehemu ya kalenda ya FIFA lakini pia, maandalizi ya kuelekea fainali hizo za Afrika.



