Ubalozi India kupokea wageni tuzo za uchoraji

UBALOZI wa India Tanzania umesema unatarajia kupokea wageni zaidi ya 1,000 wakiwemo wanafunzi wa shule shiriki, wazazi wao, na wageni mashuhuri kwenye utoaji wa tuzo kwa washindi wa uchoraji.

Awali, ubalozi huo ulisema lengo la shindano hilo ni kuhamasisha wanafunzi kukuza ubunifu wao, kujieleza kupitia sanaa, na kuthamini mchango wa sanaa katika jamii.

Amesema Shindano hilo limewapa wanafunzi jukwaa la kuonesha vipaji vyao na fursa ya kupata umaarufu kupitia maonesho.

Akizungumzia tuzo hizo Balozi wa India nchini,Bishwadip Dey, amesema kabla ya maandalizi ya tuzo hizo ubalozi uliandaa shindano la kipekee la uchoraji lililojulikana kama ‘Tanzania On Canvas’, ambalolilikishirikisha wanafunzi 30 kutoka shule 10 maarufu jijini Dar es Salaam.

“Shule zilizoshiriki ni Academic International School, Aga Khan School, Al Muntazir International School, Genesis School, Braeburn International School, Indian School Dar es Salaam, HOPAC, Dar International Academy, Feza International School, na Shaaban Robert School na kila shule iliwakilishwa na wanafunzi watatu waliobobea katika sanaa ya uchoraji na walitumia dakika 15 kukamilisha zoezi hilo,”amesema Dey.

Ameongeza,”Kama alivyosema msanii mashuhuri Pablo Picasso, Kila mtoto ni msanii changamoto ni jinsi ya kuendelea kuwa msanii ukubwani.Kupitia tukio hili, ubalozi unalenga kuhamasisha wanafunzi kuendeleza vipaji vyao vya sanaa na kuwawezesha kufuata ndoto zao,”amesema.

Amesema baada ya tuzo hizo, kutakuwa na maonyesho ya uchoraji Ubalozini hapo kwa muda wa siku 30, ambapo wanafunzi na umma kwa ujumla watapata fursa ya kushuhudia vipaji mbalimbali.

“Mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atapata Sh milioni 2.5, wa pili milioni 2,wa tatu milioni 1.5,washindi wa tuzo za faraja watapata milioni 1 kila mmoja na washiriki wengine watapata Sh 100,000 kama zawadi na kutambua juhudi zao,”amesema Dey.

Dey alisisitiza umuhimu wa sanaa inavyounganisha watu katika dunia ya leo navyozingatia zaidi mali. Aliwahimiza wanafunzi kuendelea kukuza vipaji vyao vya ubunifu sambamba na masomo yao, na kushiriki kwenye shindano kwa furaha bila hofu ya kushindwa, kwani ni fursa bora kwa maendeleo yao binafsi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button