TAASISI ya Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA) imefanya maadhimisho ya miaka yake 10 mjini Iringa katika tukio ambalo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo ameweka wazi kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho za kuboresha sheria za usalama barabarani.
Akizungumza na mabalozi na wadau wa usalama barabarani walioshiriki maadhimisho hayo, Sillo alisema mabadiliko ya sheria yanakuja ili kukabiliana na changamoto za ajali za barabarani zinazotokea mara kwa mara katika maeneo tofauti nchini.
Naibu Waziri alipongeza jitihada za RSA akisema, “Kundi hili lilianza na watu chini ya 10, lakini leo hii, lina zaidi ya wanachama 200,000 nchini, na wafuasi zaidi ya 200,000 mitandaoni. Hawa ni wazalendo wa kuigwa, wanajituma bila kujali faida, wakijitolea muda na rasilimali zao kwa ustawi wa jamii yetu.”
Katika hotuba yake, Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa kuongezwa kwa juhudi katika kufikia kundi la akina mama, ambalo alisema ni muhimu sana katika kulinda watoto dhidi ya ajali za barabarani.
“Tuongeze nguvu kufikia kundi la akina mama, ambao ni msaada mkubwa katika kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ajali,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya RSA, Kamishna Msaidizi wa Polisi (DCP), Mohamed Mpinga alisisitiza umuhimu wa mabalozi hao, akilihakikishia Jeshi la Polisi na wadau wake kuwa kazi wanayoifanya hailengi kuchukua majukumu ya polisi, bali ni kuongeza nguvu katika vita dhidi ya ajali za barabarani.
“Taasisi hii inachangia kwa kiasi kikubwa kutoa taarifa zinazolenga kuchukua hatua ili kupunguza ajali za barabarani, na mabalozi wake ni watu wazalendo ambao wanatoa huduma bila malipo yoyote,” alisema Mpinga.
Akielezea umuhimu wa mabalozi hao, Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Usalama Barabarani nchini na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Michael Deleli aliipongeza RSA akisema imekuwa ikitoa taarifa mbalimbali kuhusiana na ajali, uvunjifu wa sheria za barabarani, na makosa mengine ya usalama wa barabarani.
Alimwakilisha Mkuu wa Usalama Barabarani nchini, ACP Deleli alisema uwepo wa RSA ni muhimu kwa jeshi lao katika kukabiliana na makosa changamoto za barabarani na akaahidi kuendelea kushirikiana nao.
Katika risala yao iliyosomwa na Mtendaji Mkuu wa RSA, Augustus Fungo mabalozi hao walionyesha changamoto ya sheria za sasa, wakisema kuwa faini ndogo zinachangia madereva kutojali na kuendelea kuvunja sheria za barabarani.
“Ni wakati muafaka kwa sheria kuboreshwa na kufanyika marekebisho ili kuongeza nidhamu barabarani,” alisema.
Akizungumzia jinsi RSA inavyojiendesha, Fungo alibainisha kuwa mabalozi hawa wanajitolea kuchangia fedha kwa ajili ya kuendesha taasisi hii, jambo aliloliona kama uzalendo wa hali ya juu kwa nchi na taasisi hiyo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa (RPC), ACP Allan Bukumbi aliwashukuru mabalozi hao na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wanaotoa katika kupunguza ajali za barabarani.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Salimu Asas alisema mabalozi hao ni rasilimali muhimu kwa taifa, na mchango wao unapaswa kupongezwa.
“Tunajivunia kuwa miongoni mwa wadhamini wa RSA. Mabalozi hawa ni mfano wa uzalendo wa hali ya juu, na ni watu ambao kila mmoja wetu anatakiwa kuwaunga mkono,” alisema.
Katika sherehe hizo, mabalozi hao wametoa elimu na walihamasisha madereva kuepuka kutumia vilevi, na kuzingatia sheria za barabarani ili kulinda maisha yao na ya watumiaji wengine wa barabara.
Aidha waligawa misaada kwa waathirika wa ajali na kutoa kadi za bima ya afya kwa kaya 50.