Uchaguzi mkuu watawala ibada Pasaka

WAKRISTO jana wameadhimisha Sikukuu ya Pasaka huku mahubiri ya viongozi wengi wa dini yakijikita kuzungumzia uchaguzi mkuu, upendo, umoja, utulivu, amani na kuliombea taifa.

Askofu wa Jimbo Katoliki Ifakara, Salutaris Libana amewataka Watanzania kubadilika na kuishi maisha ya upendo na kuacha dhambi kwani si mafundisho ya Pasaka.

Askofu Libana alisema hayo jana alipokuwa akitoa ujumbe wa Pasaka wakati wa ibada ya Pasaka Kitaifa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Andrea Mtume, Jimbo Katoliki Ifakara mkoani Morogoro.

Aliwataka Wakristo wajiepushe na vishawishi vya dunia, wasikubali kusafiri wenyewe kimaisha kwa sababu watashindwa kama alivyoshindwa Adamu na Hawa, badala yake wamchague Kristo katika safari ya maisha yao.

Askofu Libana aliwataka Watanzania kudumisha amani na utulivu uliopo kwa kuzidisha upendo kwa sababu amani ni zaidi ya kukosekana kwa vita na sharti iendane na upendo.

“Sisi kama nchi tunafurahia amani, tunasema tuna amani na ni kweli tuna amani kwani hatuna vita, hatuna magomvi… amani iendane na upendo, amani iwe zao la ukweli na amani inatokana na upendo, amani inahitaji sana makubaliano na maelewano,” alisema.

Ameitaka jamii kubadilika kwa kushika yaliyoamrishwa na Mungu na kuacha yote mabaya kama mafunzo ya Pasaka yanavyofundisha kwamba wakiacha kumtazama na kumfuata Mungu basi Pasaka haitakuwa na maana.

“Tuendelee kumuabudu na kusali na kikubwa zaidi tubadilike tutoke katika tabia zetu mbaya tuishi maisha ya kipasaka, maisha ya kutokuwa na dhambi. Tuishi maisha ya yule aliyekuja kutukomboa, tubadilike mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa ujumla,” alisema.

Aliwaomba Wakristo wote nchini kuliombea taifa wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi ili Kristo asaidie ufanyike kwa njia ya amani na utulivu na Roho Mtakatifu awalete viongozi aliowaandaa ili waendeleze taifa.

Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka Watanzania kuwa na uvumilivu wa kidini ili taifa liendelee kuwa na amani na utulivu.

Askofu Pengo alisema hayo jana kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya Pasaka iliyofanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Benedicto Abate Wazo Hill, Kinondoni mkoani Dar es Salaam na kuongeza kuwa ikiwa Watanzania hawatavumiliana kiimani itakuwa hatari.

Katika mahubiri yake, Askofu Pengo aliwakumbusha waumini kuwa imani ya mtu inatokana na kile nafsi yake ilichokiamini, hivyo si sawa kwa mtu wa imani tofauti kulazimisha imani zingine zifuate fulani.

“Lakini kwa sababu imani ya kidini ni jambo ambalo tunafunuliwa na Mwenyezi Mungu hatupaswi kuwashangaa wenzetu ambao hawakubaliani na imani yetu,” alisisitiza.

Alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuheshimu imani za watu wengine na kueleza kuwa katika maisha ya kumjua Kristo hakuna haja ya mtu kuanza kujieleza kuhusu imani yake kwani kitu pekee kinachoweza kueleza imani ya mtu ni matendo yake.

Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi ambaye pia, ni Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Wolfgang Pisa akizungumza katika mkesha wa Pasaka uliofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Andrea Kagwa, Jimbo Katoliki Lindi ametaka kuliombea taifa ili liweze kupata viongozi wa haki na wazalendo katika uchaguzi wa mwaka huu.

Aliitaka serikali kusikiliza sauti na vilio vya Watanzania kwani anaamini serikali ni sikivu.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk Fredrick Shoo, ametoa wito wa maridhiano ya kweli, uchaguzi huru na haki pamoja na kuheshimiwa uamuzi wa wananchi.

Akizungumza katika ibada ya Pasaka katika Kanisa Kuu la Moshi Mjini, Askofu Shoo ameonya dhidi ya kurudia makosa ya chaguzi zilizopita, akitaka uchaguzi wa mwaka huu uwe wa wazi na unaoheshimu demokrasia.

“Jeshi letu la polisi tunawapenda sana, katika Uchaguzi Mkuu huu, tuwaombe kila mmoja na dhamira yake muwe makini msitumike vibaya na watu ambao hawaitakii mema nchi hii,” alisema Dk Shoo.

Kutoka Musoma, Padri Chukwuemeka Ngozi Anyanwu wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Nyamiongo, amewataka Wakristo kuendeleza matendo mema, kudumisha amani na kuepuka vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Padri Anyanwu alisema kipindi cha Kwaresma kilichomalizika ni mfano wa kuigwa wa mshikamano, upendo na maombi kwa ajili ya taifa hivyo kuwataka waumini waendelee kuyaishi mafunzo hayo kwa vitendo kwa kuepuka kushiriki katika vitendo vya rushwa, chuki na uchochezi.

“Ni wajibu wetu kama Wakristo kuwa mfano bora wa kuigwa, amani ya nchi yetu inategemea matendo yetu, tujiepushe na lugha za uchochezi, tuombee uchaguzi uwe wa amani na haki,” alisema Padri Anyanwu.

Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bugando Mission mkoani Mwanza, Pantaleo Cuhas amewataka Watanzania kutanguliza upendo, amani na mshikamano ili kuiwezesha nchi kushiriki na kufanikisha uchaguzi mkuu ujao. Aliwataka viongozi watakaochaguliwa kutanguliza masilahi ya wananchi.

Alisema Watanzania endapo watashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuongozwa na kusukumwa na upendo wa Mungu na si wa kibinadamu, wa kujali na kutanguliza maslahi ya watu wengine na kuondoa ubinafsi, uchama na ukabila uchaguzi huo utakuwa wa huru na haki na kuleta tumaini jipya.

Alisema kuwa Watanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini, wana kazi ya kuombea uchaguzi huo ili uweze kuwa wa mafanikio kwa masilahi ya nchi.

Aliwataka Watanzania kuwaombea watu wenye dhamana ya kuratibu uchaguzi na wale wote wanaoomba kuchaguliwa katika nafasi za uongozi na wapigakura ili kwa pamoja watangulize upendo, kutenda kwa maslahi ya taifa.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassalla amesema kuwa giza la imani ya kweli ndio imekuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la matukio ya ukatili na ubaguzi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Alisema kwa siku za karibuni, kumekuwapo na matukio mengi ya ukatili, wizi na mauaji yanayotokana na wivu wa kimapenzi ambapo kiimani, inaakisi uhalisia kuwa familia nyingi zina giza la imani ya kweli.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa akihubiri katika Kanisa Kuu la Azania Front, Dar es Salaam, aliwataka Wakristo kuitumia Pasaka kujitathmini na kujihoji pale ambapo imani zao zimefifia ili kuziimarisha.

“Sikukuu hii ni sikukuu muhimu sana katika maisha yetu ya ibada. Ni sikukuu ya kila mmoja kujihoji pale ambapo imani yako ilianza kufa, pale ambapo dhambi ilianza kujiinua ni sikukuu ya kujihoji,” alisema.

Alisema, “hatuna sababu ya kusherehekea Pasaka ambayo haigusi mioyo yetu na ambayo haigusi maisha yetu ya kiimani, leo Yesu amefufuka tufufue na maisha yetu ya kiimani.”

Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi mkoani Kilimanjaro, Ludovick Minde katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, lililoko Moshi, mkoani Kilimanjaro, alisema, “Ufufuko wa Yesu Kristo ambao tunauadhimisha leo hii, ni msingi mkuu wa imani yetu, hivyo tumuombe Mungu atuzidishie imani ili mema yote tuliyoyaishi wakati wote wa Kwaresima tuyaendeleze wakati wote wa maisha yetu badala ya kungojea kufanya hayo wakati wa kipindi maaluma cha toba tu”.

Wakati huo huo, waumini wa Kanisa la Anglikana wametakiwa kufuata miongozo ya sheria na upendo katika kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kuu Anglikana, usharika wa Mtakatifu Albano, Dar es Salaam, Canon Kahemele alisema hayo jana kanisani hapo.

“Natamani kila anayejihusisha na mchakato wa uchaguzi akiwa mgombea au mpigakura aongozwe na afuate sheria na upendo ili upendo wa Mungu udumu ndani yetu hata baada ya uchaguzi,” alisema Kahemele.

Alisema wakiishi katika misingi ya kufuata sheria za Mungu watashuhudia kicheko na furaha katika familia, watu wakitafuta msamaha, wakioneshana upendo na kusaidiana wakati wote kwa sababu matendo hayo yameandikwa katika sheria ya Mungu.

Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze, Mtume Boniface Mwamposa, wakati wa ibada maalumu ya Pasaka mkoani Dar es Salaam jana aliitaka jamii kuombea taifa amani kuelekea uchaguzi mkuu.

Alisisitiza kuwa jambo la msingi zaidi kulilinda ni amani.  “Tutaendelea kuliombea taifa, kila mmoja ainue taifa hili kwa maombi. Yesu anaitwa Mfalme wa Amani, na ukiona tumekaa hivi na kusherehekea kufufuka kwa Yesu, tambua Mungu ametupa amani,” alisema.

Alisema Yesu alifufuka ili kuleta tumaini, amani na uzima, hivyo Watanzania wanapaswa kusimama katika misingi hiyo. Alisisitiza kuwa uchaguzi usiwe sababu ya kugawanyika bali uwe fursa ya kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Imeandikwa na John Nditi (Morogoro), Naziah Kombo, (Musoma), Yohna Shida (Geita), Nashon Kennedy (Mwanza), Heckton Chuwa (Moshi) na Selemani Nzaro, Eva Sindika, Lidya Inda, Rehema Lugono, Prisca Pances (Dar).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button