UCHUMI wa Mkoa wa Mtwara umeendelea kuimarika na kufikia Sh trilioni 5.2 msimu wa mwaka 2023 kutoka Sh trilioni 4.7 msimu wa mwaka 2022.
Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa ziara ya kimafunzo ya wiki moja kwa Wakufunzi na Washiriki wa kozi ya 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema hali hiyo imesaidia kuongeza pato la wananchi kupanda kutoka Sh milioni 2.7 msimu wa mwaka 2022 mpaka Sh milioni 3.04 misimu wa mwaka 2023.
Ziara hiyo ina lengo la kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo kilimo, biashara, viwanda, uchumi, siasa pamoja na hali ya usalama kwa ujumla mkoani humo.
Aidha amesema kuwa, taarifa hiyo ya kupanda kwa uchumi huo mkoani humo ni kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) tawi la Mtwara.
” Kwahiyo unakuta uchumi wetu sisi unazidi kukua hivyo tunatoka shukrani kwa wananchi wetu wote katika kushirikiana na serikali kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa mazuri na wao kujiwekea shughuli zao za kiuchumi kufanyika vizuri zaidi”amesema Sawala
Kwa Upande wake Mkufunzi Mwandamizi Elekezi Jeshi la Anga kutoka Chuo hicho cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, Brigedia Jenerali Erick Mhoro amesema chuo hicho kimechukuwa maamuzi ya kuja kwenye mkoa huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ni pamoja na mafanikio yaliyokuwepo mkoani humo.
“Mkoa wa Mtwara ni mkoa ambao upo kimkakati katika nchi yetu ya Tanzania na una vivutio vingi ambavyo wana chuo hiki cha NDC wanatakiwa kujifunza tukianzia upande wa mazao ya biashara kama vile korosho ambayo imekuwa na mafanikio makubwa sana kwa msimu huu korosho”amesema Mhoro
Ameongeza kuwa “Mkoa wa mtwara umezalisha mapato makubwa ambayo kwa taifa yana maanisha yatakuwa chachu kwa maendeleo ya maeneo mengine”
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Kanali Herry Masokola amesema maendeleo hayo yanayoenekana mkoani humo ni uthibitisho wa sera mzuri ambazo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeziweka kwa ajili ya kuhakikisha nchi inaendelea.