Uchumi watawala ahadi za Samia, aanza ziara Unguja
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan leo anaanza kampeni katika mikoa Mjini Magharibi, Kusini Unguja na Kaskazini Unguja visiwani Zanzibar.
Samia tayari amefanya kampeni kwenye mikoa 10 ya Tanzania Bara akimalizia Kigoma baada ya kuomba kura Singida na Tabora.
Alizindua kampeni Dar es Salaam na baada ya uzinduzi akaomba kura katika mikoa ya Morogoro, Dodoma,
Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.

Singida
Akiwa Singida, Samia aliomba kura na akaahidi kutekeleza miradi ya kuufungua mkoa huo kibiashara na
kiuchumi.
Alisema kuanzia mwaka 2021, Singida ilipokea takribani Sh trilioni 1.7 kwa ajili ya maendeleo, hivyo akichaguliwa CCM itahakikisha inakamilisha miradi iliyoanza na kuanzisha miradi mingine.
SOMA: Dk Samia kuendelea na kampeni kesho Singida
Samia alitaja baadhi ya miradi kuwa ni ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa Soko la Kimataifa la Vitunguu na ujenzi Soko la Machinga Complex.
Alisema pamoja na kuwa kwa sasa Mkoa wa Singida una viwanda tisa, wananchi wakimchagua ataanzisha kongani ya viwanda itakayochangia upatikanaji wa ajira na kuongeza thamani mazao yanayozalishwa Singida.
Pia, alisema serikali itaangalia uwezekano wa kujenga kiwanja cha ndege ndani ya Singida ili kufungua fursa za kibiashara.

Samia alisema kwa kuwa Singida inasifika kwa kilimo, serikali yake itaendelea kuboresha na kujenga skimu za umwagiliaji ili wakulima walime mara mbili.
Alisema mpaka sasa imepelekea Sh bilioni 81.1 kwa ajili ya kukarabati na kujenga upya skimu za umwagiliaji zilizonufaisha wakulima 12,167 kutoka vijiji 67 vya mkoa huo.
“Tunapoendelea mbele, mkitupa ridhaa tutaendelea kuwezesha upatikanaji wa ruzuku ya mbolea na kuanzisha vituo vya ukodishaji zana za kilimo kwa bei nafuu,” alisema.
Pia, alisema serikali imeendelea kuboresha mifumo ya kuuza mazao, lengo kuu likiwa kuhakikisha usafirishaji mazao na mkulima moja kwa moja na kuondoa madalali waliokuwa wakimnyonya mkulima.
Kuhusu kituo chakupoozea umeme, Samia alisema utatekelezwa kupitia Mradi wa Grid Imara ambao unatarajia kuanza kutekelezwa mwakani, huku mradi wa kuzalisha umeme wa jua wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 80 tayari kazi ya upembuzi yakinifu umekamilika.

Tabora
Akiwa mkoani Tabora, Samia alisema serikali ya CCM itatetekeleza miradi ya maendeleo kwa nguvu kubwa zaidi kama ilivyofanya miaka mitano iliyopita.
Alisema katika wilaya za Urambo na Kaliua, umeme ulikuwa hautoshelezi mahitaji, serikali iliahidi kujenga kituo cha kupooza umeme na sasa tatizo hilo limemalizika.
Samia alisema serikali itajenga kituo cha kudhibiti mifumo ya usambazaji umeme eneo la Ziba wilayani Igunga ili kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji itakapokamilika, vituo hivyo vitadhibiti, kupooza na kusambaza
nishati hiyo.
Aliahidi kufanya upanuzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege Tabora, kazi ambayo imefikia asilimia 95 huku kiwanja kikiendelea kutumika.
Samia alisema serikali yake itaweka mkazo katika kutoa ruzuku kwa wakulima kuanzia mbolea, pembejeo na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa skimu za kumwagilia ili wakulima waweze kuzalisha mara mbili kwa mwaka.
Pia, aliahidi kutoa ruzuku kwenye chanjo za mifugo, kuboresha minada, ujenzi wa majosho na kutoa zaidi chanjo ya mifugo.
Alisema mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Dodoma na ule wa miji 28, utamaliza changamoto ya maji ndani ya mkoa huo.
Samia alisema miradi ya kitaifa inayopita katika Mkoa wa Tabora likiwemo Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) na SGR itazalisha fursa za ajira hasa kwa vijana.
“Kwa hapa Tabora Manispaa nina furaha kuwajulisha kuwa tunakuja na ujenzi wa barabara mpya ya mzunguko ya mjini Tabora, tumeshaifanyia tathmini itakayokuwa na urefu wa kilometa 82, ili kuhakikisha magari yote yasiyokuwa na ulazima kupita ndani ya Mji wa Tabora, yapite katika barabara hiyo ya nje,” alisema.
Aliongeza: “Tunataka Tabora yenye historia kubwa iwe na hadhi kubwa pia. Katika hatua nyingine ndani ya Mkoa wa Tabora, tunakwenda kujenga madaraja 133”.

Kigoma
Akiwa Kigoma, Samia alisema ahadi ya CCM na serikali kwa wana Kigoma ni kuutoa mkoa huo kutoka kuwa wa pembezoni na kuufanya wa kimkakati na kitovu cha uchumi na biashara.
“Siku za nyuma tulishazoea kusema Kigoma ni mwisho wa reli, lakini kwa kasi ya maendeleo ninayoyaona sasa, mkoa huu utakuwa kitovu cha uchumi na biashara.”
“Hili ni dhahili linaonekana. Kigoma sasa si mkoa wa pembezoni, bali ni mkoa wa kimkakati. Sio mwisho wa reli tena, bali ni kitovu cha biashara na maendeleo. Kwa uwezo wa Mungu tutalifikia hilo,” alisema.
Samia alisema ili kufikia lengo hilo kuu, aliahidi kutekeleza maeneo kadhaa ya kimkakati pindi watakapopewa ridhaa na wananchi ya kuongoza nchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni sekta ya miundombinu ya usafirishaji ambayo ni eneo lenye umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi na kusisitiza kuwa serikali yake itajizatiti kuufungua Mkoa wa Kigoma kwa njia zote za barabara, anga, reli na njia ya maji.
Samia alisema uboreshaji wa kiwanja cha ndege unaendelea, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa kitaifa wa kufungua anga la Tanzania na kuimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambalo ndege zake zinatua pia Kigoma.
Pia, Kigoma ni sehemu muhimu ya SGR, kwani inaguswa na vipande viwili vya ujenzi wa reli hiyo ikiwa ni kipande cha sita cha Tabora-Kigoma na cha saba cha Uviza-Msongati nchini Burundi, kisha itakwenda Mashariki mwa DRC.
Ahadi nyingine ni ya kuboresha Reli ya zamani ya MGR kwa kununua vichwa vipya vya treni vitatu, mabehewa mapya 22 ya abiria na mabehewa ya mizigo 44 huku mabehewa 350 ya mizigo na 33 ya abiria yakifanyiwa ukarabati.
Kwa Ziwa Tanganyika hususani Mkoa wa Kigoma, aliahidi kuendeleza ujenzi na ukarabati wa bandari za Ujiji, Kibirizi, Kabwe na Kigoma.
“Mkitupa ridhaa tutatekeleza mradi mwingine mkubwa wa kuunganisha reli na usafiri wa meli, ambapo tayari tumesaini mikataba mitatu ya ujenzi wa kiwanda cha ujenzi wa meli ambao umeshaanza kutekelezwa eneo la Katabe mkoani Kigoma,” alisema.
Ahadi nyingine ni ya ujenzi wa meli mbili za mizigo, ambapo moja ni kwa ajili ya Ziwa Tanganyika na nyingine kwa ajili ya Ziwa Victoria.
“Na ya hapa Ziwa Tanganyika itakuwa na uwezo wa kubeba tani 3500 itakayokuwa na ghorofa moja,” alisema.
Aliongeza: “Meli hizo maalumu zitapokea shehena ya mizigo inayosafirishwa na Reli ya SGR kutoka bandari za Bahari ya Hindi, hata kama ipo Bandari ya Mtwara kwa sababu tumeiweka maalumu kwa ajili ya pembejeo za kilimo, tutashusha kule zije Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwa SGR kwenda mikoa mingine. Huo ndiyo mpango wa serikali katika usafirishaji kwa njia ya maji.”
Kuhusu miundombinu ya barabara, Samia alisema serikali itahakikisha miradi yote ya barabara inayoendelea inakamilika ikiwemo vipande vyote vilivyosalia vya barabara kuu kutoka Manyovu hadi mpakani na zilizoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi.
“Ahadi nyingine ni kuhakikisha barabara za vijijini ambazo hazipo katika mpango wa kuwekewa lami, zinajengwa kwa changarawe kuzifanya zipitike misimu yote.”
Samia alisema serikali inatekeleza mradi wa Mto Malagalasi ambao utazalisha megawati za umeme 49.5 kisha kujengwa msongo wa kilovoti 132 kutoka Malagarasi hadi Kidahwe wenye urefu wa kilometa 54.
“Uwepo wa umeme wa kutosha ndani ya Mkoa wa Kigoma utajenga mazingira rafiki ya kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali na hatutasahau suala la kongani za viwanda kwa vijana kuongeza thamani mazao yanayozalishwa hapa,” alisema.
Samia aliahidi kwamba serikali yake itahakikisha taifa linajitosheleza kwenye suala la mafuta ya kupikia kwa kujielekeza kwenye kilimo cha michikichi kwa nguvu kubwa na kutoa ruzuku ya miche ya chikichi inayohitajika na kuweka kongani ya viwanda.
Pia, Samia aliahidi kuendelea na ujenzi wa majosho, mabwawa ya kunyweshea mifugo, chanjo na machinjio katika sekta ya mifugo sambamba na kutoa mikopo kwa ajili ya boti za uvuvi na vizimba.
Alisema kwasasa imewezesha uwepo wa vizimba 26 na boti mbili za uvuvi.
Kuhusu wajasiriamali, Samia aliahidi kuendelea kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali kwa mitaji kupitia Sh bilioni 200 ambazo zitatengwa na serikali yake sambamba na kutimiza ahadi ya muda mrefu ya kuboresha vibanda vya wamachinga eneo la Kibirizi.
Pia, ameahidi kuimarisha Bwawa la Katubuka ambalo linachangia mafuriko, hususani katika Kata ya Katubuka.



